Sambaza....

Mshambuliaji wa zamani wa Barcelona Samuel Eto’o amesema Lionel Messi ndiye mchezaji bora wa soka wa muda wote licha ya kushindwa kutokea katika orodha ya majina matatu yanayowania tuzo za mwanasoka bora wa Ulaya na zile za shirikisho la soka ulimwenguni ‘FIFA’ zilizotolewa jana.

Eto’o ambaye alicheza na Messi kati ya mwanza 2004 hadi 2009 akiwa katika klabu ya soka ya Barcelona amesema anapaswa kupewa heshima yake kama mchezaji bora wa dunia wa muda wote aliyewahi kutokea.

“Kwa sisi wote Leo ataendelea kubaki kama mchezaji bora wa dunia wa muda wote, binadamu walitakiwa kuchagua na wamechagua majina matatu ambao na wao wamefanya vizuri mwaka huu, lakini kwa watu kama mimi na wengine, haitabadilisha ukweli kwamba Leo ni mchezaji bora wa dunia wa muda wote,” Eto’o amesema.

Katika tuzo za FIFA zilizofanyika jijini London jana usiku, Lionel Messi alitajwa kuwepo kwenye kikosi bora cha mwaka (FIFPro World XI) licha ya kutojumuishwa kwenye majina matatu yaliyokuwa yanawania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka.

Katika tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa FIFA, nyota wa Real Madrid na timu ya Taifa ya Croatia Luka Modric alichaguliwa mbele ya Cristiano Ronaldo wa Juventus na Mohamed Salah wa Liverpool.

Messi ameshinda mataji tisa ya ligi kuu nchini Hispania (LaLiga), Mataji manne ya Ligi ya mabingwa Ulaya (UEFA Champions League), Tuzo tano za Ballon d’Or, pamoja na tuzo mbalimbali katika maisha yake ya soka.

Sambaza....