Kiraka wa Klabu ya Simba Erasto Edward Nyoni leo amekiona chamoto katika mazoezi ya kwanza tangu kurejea kwa timu kutoka Algeria baada ya benchi la ufundi kumuweka kitimoto kabla ya mazoezi katika uwanja wa Bokko Beach Ununio.
Baada ya kupona majeraha yake aliyoyapata katika michuano ya Mapinduzi Zanzibar na kumuweka nje takribani wiki nane Erasto Nyoni alisharuhusiwa kuanza mazoezi mepesi ili aweze kuungana na wenzie na kufanya mazoezi ya nguvu na kikosi.
Erasto Nyoni aliwekwa kitimoto na benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Patrick Aissems huku pia wakiwepo Kocha wa viunga Zrane, meneja wa Simba Patrick Rweyemamu na kocha msaidizi Deniss Kitambi.
Erasto Nyoni ilimchukua dakika 20 kujielezea mbele ya uongozi huku sababu kubwa ikionekana ni ukosefu wa nidhamu. Baada ya Simba kuelekea nchini Algeria na Erasto Nyoni kubaki Dar aliachiwa program ya mazoezi lakink hakuifanya inavyostahili kama alivyoachiwa na mganga wa timu. Lakini pia Erasto Nyoni alikua akitafutwa kwa kupigiwa simu na uongozi lakini alikua hapatikani kwa maana alikua amezima simu yake ya mkononi.
Pengine kiwango hafifu alichokionyesha beki Paul Bukaba katika mchezo dhidi ya JS Saoura ndicho kimefanya benchi la ufundi kuhitaji urejeo wa Erasto Nyoni haraka.