Pengine ni kawaida yetu Watanzania kutupia macho kwa mapacha wawili wa Kariakoo, pengine ni utaratibu wa baadhi ya nchi kutotupia macho kwenye vipaji vya madaraja ya chini.
Nimeshuhudia wachezaji wengi wanaocheza kwenye zile timu zetu kubwa wakiwa na uwezo wa kawaida tu huku vipaji maridhawa vikiwa vinaoza mikoani au timu za madaraja ya chini.
Timu zetu kubwa zinahaha kutafuta wachezaji wa kuweza kuzipatia mafanikio zikitoka hadi nje ya nchi kutafuta vipaji maridhawa lakini inashangaza hawavioni vipaji vilivyopo japo ni vichache.
Edward Songo, mwajiriwa wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania na mchezaji hatari wa JKT Tanzania ni moja ya tunu nzuri ya Taifa hili ambayo “wenye mpira wao” wameamua kutomtazama kwa karibu na kukilinda kipaji hiki maridhawa, ni nadra kupata mchezaji anaekupa mambo zaidi ya mawili akiwa uwanja kwa wakati mmoja, Songo ni mchezaji anaeweza kukupiga chenga huku anakimbia na hapo hapo akapiga shuti ambalo litakua lina shabaha nzuri kabisa. Sijazungumzia matumizi sahihi ya nguvu zake, vitu vyote vikifanyika katika matumizi sahihi ya mguu wa kushoto, akimudu kucheza nafasi zote za ushambuliaji.
Songo ndiye winga hatari kwa sasa nchini mzawa ambae hata timu zetu kubwa hazina winga kama huyu, ni aina ya wachezaji kama Kibu Denis lakini huyu Songo akiwa ni mchezaji wa kisasa zaidi.
Mifumo yetu mibovu ya kukuza soka ndiyo inayotukosesha bahati ya kufaidi vipaji halisi vya Kitanzania, ukimtoa Jerrison Tegete aliyeitwa timu ya Taifa sina uhahika kama iliwahi tokea kwa mchezaji mwingine kuitwa team ya Taifa akiwa hachezi Ligi kuu au nje ya nchi.
Hakika penye miti hapana wajenzi!
Na Celestine Chomola “Chomox”