Winga wa timu ya soka ya Chelsea ya England Eden Hazard amesema hastahili kuchukua tuzo ya Ballon d’Or licha ya kuwa kwenye kiwango kizuri kwa sasa lakini badala yake mshambuliaji wa Paris Saint Germain na timu ya Taifa ya Ufaransa Kylian Mbappe ndiye anayestahili.
Hazard ambaye mpaka sasa amefunga mabao saba katika michezo 12 ya ligi kuu msimu huu, akikalia nafasi ya pili katika wachezaji waliofunga mabao mengi hadi sasa, amesema hafikirii kabisa kwamba mwaka huu alichokifanya kinaweza kumpa tuzo kubwa kama Ballon d’Or.
Raia huyo wa Ublegiji amekuwa na kiwango kizuri hata kabla ya michuano ya Kombe la Dunia iliyomalizika mwezi Julai nchini Russia, lakini amejiondoa katika wale wanaofikiriwa kutwaa tuzo hiyo itakayotolewa mwezi ujao Mjini Paris.
“Ingawa nina mwaka mzuri, lakini natakiwa kuwa mkweli, sistahili kutwaa tuzo ya Ballon d’Or, nafikiri kuna wachezaji wengine ambao wamefanya vizuri zaidi yangu, kutwaa Ballon d’Or sio kipengele changu kwa sasa, kama nitashinda siku moja itakuwa vizuri lakini hata nisiposhinda hakuna tatizo,” Hazard amesema.
Alipoulizwa nani anadhani anafaa kutwaa tuzo hiyo Hazard amesema, “Unaweza kumtaja Luka Modric lakini amecheza mechi chache na kwa kiwango si kizuri sana toka mwezi Agosti Septemba, hivyo kwa sasa naweza kusema ni Kylian Mbappe,” amesema.
Mwaka 2015 katika majina ya wanaowania tuzo za Ballon d’Or Hazard alishika nafasi ya nane lakini mwaka uliopita alishika nafasi ya 19 kwa wachezaji bora duniani.