Mlinda mlango nambari moja wa Manchester United David De Gea ametanabaisha kuwa wachezaji wenzake na benchi zima la timu halina furaha kama watu wengi wanavyodhani licha ya kuwa na muendelezo mzuri toka aondoke kocha Jose Mourihno.
De Gea amesema sifa kubwa ya klabu ya Manchester United ni kuwa mabingwa na kukaa kileleni, lakini kwa vile bado wapo nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi wakiwa nyuma ya Liverpool kwa alama 16 haliwapi furaha kabisa.
“Tunafuraha na namna timu inavyoshinda kila mchezo, lakini hatujaridhika na hali nzima ilivyo, hii ni klabu ambayo inatakiwa kuwa katika mapambano ya kuwania ubingwa, kwa sasa tunataka kurudi kwenye nafasi itakayotupa ushiriki wa michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya, ni ngumu lakini tumeweza kupunguza tofauti ya alama angalau kidogo,” De Gea amesema.
Kabla ya kuondoka kwa Jose Mourihno Manchester United walikuwa katika nafasi ya sita kama ilivyo sasa lakini walikuwa mbali kwa alama 11 dhidi ya Chelsea ambaye yupo kwenye nafasi ya kushiriki ligi ya mabingwa lakini kwa sasa zimebaki alama tatu pekee.
Baada ya kuingia hatua inayofuata ya mashindano ya chama cha soka England (FA CUP) kwa kuwachapa Arsenal kwa mabao 3-1, Manchester United watakuwa na kibarua kizito siku ya Jumanne watakapowaalika Burnley kwenye mchezo wa ligi.
“Ni timu nzuri hasa wanapokuwa wanataka matokeo, na tuna muendelezo mzuri mpaka sasa, watajaribu kututia hofu kwa mipira yao mirefu na ni hatari sana linapokuja suala na mipira iliyokufa, lakini sisi tunacheza nyumbani” De Gea amesema.
Rekodi
zinaonesha mara ya Mwisho kwa Manchester United kushinda dhidi ya Burnley
ilikuwa ni mwaka 2015 na michezo miwili iliyopita Burnley wamefanikiwa kutoa
sare kwenye uwanja wa nyumbani wa Manchester United, Old Trafford.