Mechi nane zilizopita alizokutana na Chelsea hajafanikiwa kufunga hata goli moja.Hii haiwezi kuondoa ubora na umuhimu wa Lionel Messi katika kuamua matokeo ya mechi ya leo. Amekuwa kimya kwa muda mrefu sana, ukimya ambao umesababisha asiwe rafiki wa nyavu kwa michezo mitano iliyopita.
Ukimya huu usikufanye kukuaminisha kuwa amekuwa kipofu na kuwinda kwake hakuwezi kuwa na manufaa. Yeye ndiye amekuwa funguo muhimu kwenye uamuzi wa kufungulia kufuli la mafanikio ya Barcelona msimu huu.?
Hata kama asipofunga huifanya timu ipate ushindi kwa sababu yeye ndiye nguzo ya ushindi kwa Barcelona!, kwanini nasema hivo?
Mwalimu Ernesto Valverde msimu huu amekuwa akitumia mifumo mitatu ambayo ni 4-4-2, 4-3-3 na 3-5-2
Mifumo yote hii Lionel Messi amekuwa akitumika kama njia ya Barcelona kupata magoli kwa sababu kwenye mifumo hii , Lionel Messi hushuka chini katikati, anaposhuka chini kuna vitu viwili hutokea, cha kwanza ni yeye kuongeza idadi ya viungo katika eneo la katikati.
Mfano anaposhuka chini katikati katika mfumo wa 4-4-2 huongeza idadi ya viungo kuwa watano kwa sababu Ernesto Valverde hutumia 4-4-2 Diamond ambapo viungo hukaa katikati na kutengeneza uwazi katika eneo la pembeni mwa uwanja.
Kwenye mfumo wa 4-3-3 huongeza idadi ya viungo katika eneo la katikati kuwa wanne, na kwenye mfumo wa 3-5-2 pia huongeza idadi ya viungo wa katikati kuwa wanne, hii huwa na faida kubwa sana kwa Barcelona kwa sababu eneo la kiungo huwa na watu wengi dhidi ya mpinzani wake wanayekutana naye.
Kitu cha pili ambacho hutokea kama Lionel Messi anaposhuka chini katikati ni uwazi anaoutengeneza eneo la mbele , anaposhuka chini, beki wa timu pinzani hulazimika kushuka naye chini kumkaba anaposhuka chini nyuma huwa kunakuwa na uwazi ambao hutumiwa na wachezaji wa Barcelona kuutumia kufunga
Hapa ndipo umuhimu wa Lionel Messi unapoanzia katika kikosi cha Barcelona hata kama asipofunga.
Umuhimu ambao hautofautiani na umuhimu wa Eden Hazard katika kikosi cha Chelsea, msimu uliopita Antonio Conte aliwekeza nguvu na akili zake katika mfumo wa 3-4-3 tofauti na msimu huu ambapo amekuwa akitumia mifumo miwili ya 3-5-2 na 3-4-3, katika mifumo yote hii Eden Hazard hushuka chini katikati kama Lionel Messi na kuleta madhara yale yale ambayo Lionel Messi huleta kipindi ambacho anaposhuka chini.
Kwa hiyo hawa ni watu pekee (Eden Hazard na Lionel Messi) ambao wameshikilia ufunguo wa ubunifu wa upatikanaji wa magoli kule mbele.
Hawa ndiyo wamebeba dhamana kama daraja litaporomoka au kuimarika zaidi.
Pamoja na kwamba aina ya funguo za upatikaji wa magoli zipo katika miguu inayorandana, lakini kuna utofaufi kwenye ukabaji kati ya hizi timu zote mbili.
Chelsea mara nyingi ukabaji wake hauanzii juu kama ilivyo kwa Barcelona ambayo huanza kukabia juu, kukabia juu kuna faida kubwa sana kwa sababu humfanya mpinzani asianzie mipango ya kushambulia kwa utulivu akiwa eneo la nyuma kitu ambacho humlazimu kufanya makosa ambayo yanapelekea kupoteza umiliki wa mpira kutokana na presha ya kukabiwa juu.
Yapi madhaifu ya Barcelona upande wa kujilinda?
Tangu kuondoka kwa Dani Alves, eneo la beki wa kulia la Barcelona limekuwa dhaifu sana, kuna watu wawili ambao wamekuwa wakibadilishana eneo hilo (Sergi Roberto na Nelson Semedo) ambao mpaka sasa wameonesha udhaifu mkubwa kwenye kukaba, eneo hili likitumika vizuri na Chelsea linaweza likawa na faida kubwa kwao.
Yapi madhaifu ya Barcelona upande wa kushambulia?
Waweza ukachukua muda mrefu kutafakari ni eneo lipi ambalo Barcelona huwaangusha kipindi wanaposhambulia na ukatumia muda mrefu kutopata jibu kwa sababu ya ushindi ambao Barcelona wamekuwa wakiupata.
Viungo wa katikati wa Barcelona hawana wastani mzuri wa kutengeneza nafasi za magoli ukilinganisha na viungo wa Chelsea. Sergio Busquets ana wastani wa kutengeneza nafasi 0.70 katika kila mchezo, Iniesta ana wastani wa kutengeneza nafasi 0.78 kwa kila mchezo na Rakitic ana wastani wa kutengeneza nafasi 1.05 kwa kila mchezo
Wakati Viungo wa Chelsea ambao wana nafasi kubwa ya kuanza leo , wanawastani mzuri wa kutengeneza magoli kwa kila mchezo. Mfano Kante anawastani wa kutengeneza nafasi 1.33 kwa kila mchezo, wastani ambao ni mkubwa kuzidi kiungo yoyote wa kati wa Barcelona. Fabregas ana wastani wa kutengeneza nafasi 2.91 kwa kila mechi.
Upi udhaifu wa Chelsea wakati wa kujilinda?
Mwanzoni nilisema Chelsea haikabii juu, hii inaweza kumpa faida mpinzani asiwe na presha hivo kuanza mipango yake bila presha ambayo itamsababishia apoteze umiliki wa mpira.
Pili mabeki wake wa kati wawili ( Cahil pamoja na Rudiger) wamekuwa na makosa mengi binafsi yanayotokana na wao kutojipanga vizuri, makosa haya huwezi kuyaona katika mabeki wa kati wa Barcelona.
Kipi wakifanye Chelsea ili washinde mechi hii?
Tumeona viungo wa Chelsea wana wastani mzuri wa kutengeneza nafasi za ufungaji wa magoli kuliko viungo wa Barcelona, hii wanaweza kutumia kama silaha kwao na kuzitumia vizuri nafasi ambazo wanazitengeneza.
Chelsea ikiamua kukaa nyuma ya mpira na kuamua kufanya mashambulizi ya kushitukiza wanatakiwa kuwafanya Cahil na Rudiger kuwa watulivu na kuepukana na makosa mengi binafsi wanayoyafanya. Mashambulizi yao ya kushtukiza yakifanyika upande wa kulia kwa Barcelona kutakuwa na faida kubwa kwao kwa sababu upande wa kulia wa Barcelona hauko imara.
Kipi wakifanye Barcelona ili washinde kwenye mechi hii?
Kukabia juu kutakuwa na faida kwao, kwa sababu kutawafanya mabeki wa Chelsea kupata presha kubwa na ukizingatia kuwa siyo watulivu na hufanya makosa mengi kipindi presha kubwa inapokuwa kwao kutawapa mwanya mkubwa Barcelona kushinda kwa sababu wananafasi ya kupata umiliki wa mipira katika eneo lao la mbele na kuitumia vizuri hiyo mipira kwa kuanzisha mashambulizi ambayo yatakuwa na faida kubwa kwao.