Mengi yalizungumzwa sana mwanzoni mwa msimu huu ligi kuu Hispania maarufu kama La Liga, hiyo ni kutokana na ukame wa mabao aliokuwa nao mshambuliaji Cristiano Ronaldo na kutafsiriwa kuwa kiwango chake kimefikia tamati.
Kwa sasa hali imeonekana kubadilika, mara baada ya mshambuliaji huyo wa Real Madrid kufunga mabao manne katika mchezo dhidi ya Girona, hii inawezekana ikafuta ile misemo iliyokuwa awali.
Ikiwa ni Hat trick yake ya 50, tangu kuanza kucheza soka kwa nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno, pia akiwa amefunga jumla ya mabao 17, katika michezo 8 iliyopita akiichezea Real Madrid na hii takwimu ambayo inaonesha bado mshambuliaji ni moto wa kuotea mbali.
Mabao yake manne aliyofunga hapo jana, yanamfanya kufikisha jumla ya mabao 25 kunako La Liga akizidiwa kwa mabao matatu na Lionel Messi, na hii inafufua matumaini yake ya kushinda tuzo ya mfungaji bora.
Itakumbukwa mwanzoni mwa mwezi Novemba, Cristiano Ronaldo, alieleza hitaji lake la kushinda tuzo ya mfungaji bora wakati huo akiwa na bao 1 tu, huku mpinzani wake Lionel Messi akiwa ametupia kambani mabao 11 hali iliyotafsiriwa kama kichekesho, lakini kwa hali ilivyo sasa inawezekana kwake kushinda tuzo hiyo.