Janga la virusi vya Covid19 limeitikisa haswa dunia na kupelekea athari mbalimbali za kiuchumi lakini pia limeathiri kwa kiasi kikubwa kwenye idara ya michezo na moja kwa moja katika mpira wa miguu.
Kutokana na janga hilo serikali ilisimamisha Ligi Kuu na ligi nyingine zote zilizo chini ya TFF ili kuepusha mikusanyiko ambayo ingepelekea kuenea kwa virusi hivyo. Na hivyo kupelekea klabu za Ligi Kuu kuvunja kambi na kuwaacha wachezaji wake wabaki nyumbani.
Baada ya likizo hiyo fupi wachezaji wa kigeni wa Simba walitimka nchini na kwenda kuungana na familia zao katika nchi zao. Wachezaji wa Simba walioondoka na kurudi kwao ni pamoja na Luis Miquissone (Msumbiji), Francis Kahata (Kenya), Meddie Kagere (Rwanda), Sharaf Shibuob (Sudan) na Clatous Chama (Zambia).
Kwa wachezaji walioondoka katika kikosi cha Simba wengi wao wanacheza eneo la kiungo ambapo anacheza Said Ndemla ambao ni Clatous Chama, Sharaf Shiboub na Francis Kahata ambao ni wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Mbelgiji Van Debroeck.
Wachezaji hao watakua wamekumbana na wakati mgumu kurudi nchini baada ya nchi zao kufunga mipaka, hivyo haifahamiki ni lini watarejea nchini. Lakini pia serikali imetoa agizo la kukaa siku 14 karantini kwa wageni wote watakaoingi nchini.
Kwa nafasi hiyo basi ni wakati wa Ndemla kutumia nafasi hii kipindi Ligi ikiwa imesimama kujiweka sawa na kuweza kugombea namba na wachezaji hao wa kigeni ambao wamemfanya kukaa benchi muda mrefu katika ligi.
Lakini pia kutokana na kukosekana kwao kwa muda mrefu kwa wachezaji hao wa kigeni ni wazi kua Ligi itakaporudi Said Ndemla ana nafasi kubwa ya kutumika katika kikosi cha Simba katika eneo la kiungo wa kati. Kukosekana na Sharaf Shiboub na Clatous Chama ni dhahiri shahiri mwalimu Matola na Sven chaguo lao la kwanza katika eneo la kiungo watakua ni Jonas Mkude, Fraga Vieira na Said Ndemla ambao wapo kikosini kwa sasa.
Sasa ni wakati wa Said Ndemla kuonyesha uwezo wake na kumshawishi mwalim kipindi Ligi itakaporejea na hivyo kubeba imani ya mwalim na kuweza kumbakisha kikosini.
Ama kwa hakika kurejea kwa Ligi baada ya kusimama kupisha ugonjwa wa Corona kitakua ni kipindi cha neema kwa Ndemla, huku mashabiki wake wakitegemea kuona mashuti makali, pasi ndefu na pasi mpenyezo kutoka kwa Said Hamis Ndemla “Daktari”.