Sambaza....

Umewahi kufikiria Maurizio Sarri akiikosa ‘fegi’ inakuwaje? Au umewahi fikiria kuwa kama ukikosa kitu fulani ulichozoea kufanya madhara yake yanakuwaje au utajisikiaje.

Wachunguzi wa mambo wamewahi kusema binadamu anaweza kupoteza hamu ya kila kitu iwapo mazoea yake yatakuwa yamebadilika. Yaani, ni kama vile kilivyo kiti cha mzee pale nyumbani siku aje mgeni mwingine na kukikalia wakati mzee aliingia chumbani mara moja…ule utofauti wake.

Maurizio Sarri

Dunia muda huu ipo likizo kubwa na ya hatari zaidi kutokea, hii ni kutokana na kusambaa kwa kirusi cha COVID19. Kirusi hiki hatari zaidi kilianzia nchini China na sasa takribani nchi zote ulimwenguni zimeguswa. Shughuli nyingi zikiwa zimeshafungwa na ratiba mbalimbali kusogezwa mbele au kufutwa kabisa. Hakuna sekta ambayo haijaguswa na kuachwa salama mpaka muda huu.

Luis Miquissone akithibitiwa na wachezaji wa Yanga.

Ulevi wetu mimi ninayeandika na wewe unayesoma ni mpira wa miguu almaarufu Kandanda. Ligi zote maarufu na kubwa Duniani  Wikiendi zetu zimekuwa ngumu sana. EPL, La Liga na Hata Ligi Kuu yetu zimesimama. Hakuna burudani za Morisson wala Tambo za Meddie Kagere tena. Manara ni kama kaenda pia likizo, mashabiki pia wanaugulia tu maumivu ya kukosa.

Anthony Martial akishangilia na Bruno Fernandes.

”Mpwa, ni kama ninaumwa vile, maana hakuna burudani tena. Mpira upo ICU,  na mawazo yote pia yapo ICU” Tigana Lukinja akiongea na mtandao huu.

Mpira wa miguu unawaunganisha watu na kuwapa burudani, Jurgen Klop , Meneja alinukuliwa mwanzoni kabisa mwa sakata hili kuanza kuwa ni bora wasicheze mechi tu kama uwanjani hakutakuwa na mashabiki. Hapo akitambua kabisa umuhimu wa mashabiki uwanjani na baada ya gemu. Kumbuka hapo hajajumuisha wale ambao wanatazama katika luninga na vibanda umiza.

Tupo likizo ndefu sana ambayo hatujui lini itaisha, lakini sijui tunafanya nini kipindi hiki wakati hakuna Ligi maarufu. “Bro hali imekuwa ngumu sana Kibanda Umiza changu sasa naonyesha movie tu” moja ya kijana ambaye anaonyesha mechi katika luninga yake. Huyu ni sehemu ndogo ya wale ambao wameguswa kiuchumi kuhusiana na janga hili la Corona.

Lakini umegundua nini? Mpira unatutibu mambo mengi sana, muda huu watu wapweke sana hata vijiwe vimepoza sababu hakuna kutambiana kuhusu chenga za Morisson au Luis. Ndio maana wengine wakasema soka ni kama ulabu vile, ukiwa ‘addicted’ utatafuta kila mahali ili uupate.

 

Tuendelee kufuata ushauri wa wataalamu wa Afya kujikinga na virusi vya Corona, na bila shaka tutarudi tena uwanjani kama kawaida.

 

Sambaza....