Hakuna mchezaji ambae ni ghali na bidhaa adimu katika dirisha kubwa la usajili linalokuja kama mlinzi wa kati wa Coastal Union na timu ya Taifa “Taifa Stars” Bakari Nondo Mwamunyeto.
Mwamunyeto ametumia misimu miwili tu katika Ligi Kuu Bara akiwa na Coastal Union kuonyesha yeye ni nani na kuwafanya Simba, Yanga na Azam fc waanze kupigania saini yake ili kumng’oa kwa Wagosi wa kaya.
Inaelezwa thamani ya mlinzi huyo wa Stars ni milioni 70 mpaka 100, huku pia klabu inayomtaka ikitakiwa kumalizana na Coastal Union ili kuununua mkataba wake uliobaki wa mwaka mmoja.
Kitu kizuri hapa kwa Coastal Union ni kufanya biashara nzuri kutokana na mchezaji mwenyewe (Mwamunyeto). Coastal ilimsainisha miaka minne (wakati wanamsjajili) beki huyo mahiri na mpaka sasa ameitumikia miaka mitatu huku akiwa amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake.
Na hii inapelekea Coastal kusubiri mavuno ya mauzo ya fedha za Bakari Mwamunyeto kutoka kwa klabu yoyote inayomuhitaji. Inasemekana Simba waliweka dau la milioni 30 kwa Coastal ili kumsana Mwamunyeto lakini Coastal Union wamechomoa wakisema ni dau dogo.
Lakini upande wa pili Yanga kupitia GSM wanaonekana wanakaribia kufanikiwa kupata saini yake kutokana na kuelewana na uongozi wa Coastal Union juu ya kiasi cha fedha wanachotakiwa kutoa ili kununua mkataba wake. Kiasi cha shilingi milioni 50 mpaka 70 huenda kikatumika na Yanga kuwapatia Coastal Union.
Baada ya kukubaliana na Coastal juu ya dau la usajili, Yanga sasa wanageukia kwa mchezaji mwenyewe Bakari Mwamunyeto kukubaliana maslahi binafsi ili kuweza kumshawishi na kumwaga wino kwa Wanajangwani.