Klabu ya soka ya Azam imewapa mapumziko wachezaji wake hadi Jumatatu watakapoingia kambini rasmi kujiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Wanatam Tam Mtibwa Sugar, Disemba 29 mwaka huu kwenye uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.
Kubwa zaidi kuelekea katika mchezo huo ni kuwepo kwa mchezaji wa kimataifa Obrey Chirwaambaye klabu yake imethibitisha kuwa tayari wameshapata vibali vya kumruhusu kucheza soka nchini.
Jaffary Idd Maganga ni afisa habari wa Azam amesema kuwa wanatarajia Chirwa atakuwepo kwenye mchezo huo kwani wamekamilisha kila kitu ambacho kilikuwa kinatakiwa kwa mchezaji huyo kuruhusiwa kucheza soka la kulipwa nchini, ikiwemo ITC kutokaklabu yake ya Misri pamoja na vibali vya kazi kutoka ofisi za uhamiaji nawizara ya kazi.
“Baada ya kupatikana kwa ITC, pia tulikuwa tunahangaika suala la kumtafutia vibali ili kuruhusiwa kucheza hapa nchini, kwa hiyo afisa wetu anayeshughulikia suala hilo Chuma Suleiman Twalib amekamilisha baada ya vibali vyake kutoka wizara ya Kazi kuwa tayari, kinachosubiriwa tu ni kuanza kwa raundi ya pili ili awezekuonekana uwanjani,” amesema.
Chirwa ambaye aliwahi kuitumikia Yanga amejiunga na Azam akitokea Nogoom El Mostakbal Football Club ya nchini Misri na alishindwa kuichezea Azam kutokana na vibalivyake kushindwa kupatikana kwa wakati.
Chirwa anaungana na Donald Ngoma ambaye naye aliwahi kuitumikia Yanga katika safu ya Ushambuliaji ya Azam jambo ambalo Maganga anaamini kuwa litaisaidia timu hiyo kufanya vizuri katika michezo inayokuja.
“Ni matumaini yetu kuwa kuja kwake kutaongeza ubora katika eneo la ushambuliaji, kila mtu ameona uwezo wa Donald Ngoma ambaye anafunga karibu kila mechi, kwa hiyo kuja kwa Chirwa ambaye alikuwa anacheza naye Yanga kutazidisha combination pale mbele, pamoja na wachezaji wengine kama Danny Lyanga, Tafadzwa Kutinyu na makinda kama Yahya Zayd,” amesema.