Mshambuliaji wa Haruna Chanongo pamoja na Saleh Khamis wameachwa mkoani Morogoro katika kikosi cha Mtibwa Sugar ambacho kimeondoka alfajiri ya leo kuelekea mkoani Arusha tayari kwa fainali ya Azam Sports Federations dhidi ya Singida United Jumamosi ya Juni 2 mwaka huu.
Wachezaji hao wameondolewa katika kikosi hicho kutokana na majeraha lakini kwa mujibu wa katibu wa klabu hiyo Salumu Kijazi amesema wachezaji hao watawafuata wenzao pamoja na kikosi B siku ya Ijumaa.
“Timu imeondoka leo Alfajiri kuelekea mjini Arusha, vijana wote wapo timamu wako vizuri, isipokuwa kwa wachezaji wawili Haruna Chanongo na Salehe Khamis wao wamebaki na watajiunga na wenzao keshokutwa wakiwa na kikosi B, lakini wengine wote wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo wa fainali,” Kijazi ameuambia mtandao huu.
Katika hatua nyingine Kijazi amesema wanaimani kubwa ya kuchukua ubingwa wa FA msimu huu na tayari uongozi umeandaa sherehe kubwa ya kuwapokea wachezaji wao siku ya Jumapili watakaporejea na medani pamoja na kombe la ushindi.
“Kuna shamrashamra kubwa sana kwenye Tarafa ya Turiani, waendesha boda boda pamoja na wale wa Noah wamepanga siku ya jumapili kuja kutupokea kuanzia pale Korogwe kwa ajili ya maandamano ya kurudi Turiani, na hatutawaangusha tutachukua kombe,” Kijazi ameeleza.
Tayari shirikisho la soka nchini TFF limeshatangaza viingilio vya mchezo huo ambapo kiingilio cha chini kikitazamiwa kuwa shilingi Elfu Moja (1,000), huku wakiongeza zawadi ambapo sasa makamu bingwa atajinyakulia shilingi milioni 10 tofauti na misimu miwili ya awali ambapo walitoka patupu.
Ikumbukwe mchezo huo ambao utapigwa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid bingwa wake ataiwakilisha nchi katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.