Katika dakika ya 96, dakika ya mwisho ya nyongeza kati ya dakika 6 alizoongeza mwamuzi Shomari Lawi katika mchezo wa Ligi kuu Vodacom Tanzania bara kati ya Mbeya City na Yanga uliofanyika Aprili 22, 2018, Sokoine, Mbeya ulizuka utata ikidaiwa mchezaji Namba 10 wa Mbeya City aliyefanyiwa mabadiliko alirudi tena uwanjani kucheza kinyume cha taratibu na kufanya idadi ya wachezaji wa Mbeya City kuzidi uwanjani, anandika Masau Bwire, endelea hapa…
Kwakuwa mchezaji wao mmoja tayari alikuwa ameoneshwa na kutolewa nje kwa kadi nyekundu, Mbeya City walitakiwa wabakie wachezaji 10 uwanjani lakini, ikadaiwa kwamba, kwakuwa mchezaji namba 10, Eliud Ambokile aliyefanyiwa mabadiliko aliingia tena uwanjani, bado Mbeya City walicheza wachezaji 11 uwanjani badala ya wachezaji 10.
Hili ni jambo kubwa sana katika soka, jambo linakiuka taratibu na kanuni, hivyo linahitaji uchunguzi wa hali ya juu ili maamuzi yatakayotolewa na mamlaka husika yawe ya kweli na haki ya kweli.
Jambo hili halihitaji mazungumzo ya kiushabiki, ushabiki wa kuvuta kwako kuonekane ni sahihi wakati si hivyo ili mradi tu upate haki bila haki ya kuipata haki hiyo. Tukiwa katika mtazamo huo tunamkosea Mungu, tunaukosea na kuudhalilisha mpira wetu.
Mimi baada ya taarifa za uwepo wa tukio hilo, nilifanya uchunguzi wangu mdogo nikabaini yafuatayo;
Dakika ya 90+6, Mbeya City walitaka kufanya mabadiliko kumtoa mchezaji namba 10, Eliud Ambokile nafasi yake ichukuliwe na mchezaji namba 19, Danny Jerome, walitoa taarifa kwa fomu ya mabadiliko kwa mwamuzi wa akiba, Mashaka Mwandembwa ambaye naye katika ubao wa kuonesha mabadiliko aliandika mabadiliko hayo.
Kabla ya mwamuzi wa akiba kunyoosha kibao cha mabadiliko hayo, mchezaji namba 29, Frank Ikobela wa Mbeya City alianguka baada ya kuumizwa na mchezaji wa Yanga, mwamuzi wa mchezo, Shomari Lawi aliita machela kumtoa nje ya uwanja mchezaji huyo ambaye alitolewa kupitia upande wa mwamuzi msaidizi namba mbili, camera za Azam tv hazikuweza kumumlika.
Baada ya mchezaji huyo kuumia, benchi la ufundi la Mbeya City lilibadili mabadiliko waliyotaka kuyafanya, badala ya kutoka mchezaji namba 10, Eliud Ambokile, atoke mchezaji namba 29, Frank Ikobela, nafasi yake ichukuliwe na mchezaji namba 19, Danny Jerome, walitoa taarifa kwa mwamuzi wa akiba ambaye aliwataka wafanye mabadiliko hayo kwenye fomu ya mabadiliko, badala ya kutoka namba 10 kama mabadiliko ya awali yalivyokuwa, atoke namba 29 aliyetolewa kwa machela.
Mwamuzi wa akiba, Mashaka Mwandembwa, katika ubao wake wa mabadiliko ya wachezaji alibadili upande mmoja, upande mwingine akasahau kurekebisha, akaacha mabadiliko ya awali ya namba 10 atoke aingie namba 19.
Aliponyanyua ubao huo wa mabadiliko, upande wa uwanjani alionesha anatoka namba 29 anaingia namba 19 (Mabadiliko yaliyofanyika), lakini, upande wa watazamaji/camera, ubao ulionesha anatoka namba 10 anaingia namba 19, mabadiliko ambayo hayakufanyika, yaliyozua utata. (Ni makosa ya kibinadamu, yeyote anaweza kuyafanya). Hii ni kutokana na haraka iliyokuwepo kwani, mchezo ulikuwa umebakisha dakika moja katika zile sita zilizoongezwa.
Kwa taarifa nilizozipata, ambazo sijazithibitisha, baada ya camera kumlika mabadiliko ya namba 10 anatoka, anaingia namba 19, bado akaonekana kuwemo uwanjani, washabiki waliwasiliana na benchi la ufundi la Yanga kwamba, namba 10 ametolewa lakini kaingia tena kinyemera anacheza uwanjani, ndipo kocha wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali, (Rafiki yangu, nampenda tangu nikiwa mdogo) alikwenda kulalamika kwa mwamuzi wa akiba, Mashaka Mwandembwa.
Mwandembwa baada ya malalamiko hayo, alimtaarifu mwamuzi msaidizi namba moja, Omary Juma ambaye alinyoosha kibendera chake akimtaka mwamuzi asimamishe mchezo ili kufanya uhakiki wa wachezaji wa Mbeya City uwanjani lakini mwamuzi kwakuwa mpira dakika za nyongeza zilikuwa zimemalizika, kabla hajaona kibendera cha msaidizi wake namba moja, alipuliza filimbi ya kumaliza mchezo, washabiki wakavamia uwanja.
Huu ni uchunguzi wangu. Kabla hujaukubali au kuukataa, fanya wako, ujiridhishe.
Masau Bwire – Mzalendo