Sambaza....

Safari ya Wekundu wa Msimbazi Simba katika Ligi ya Mabingwa imeishia rasmi mbele ya mabingwa watetezi Wydad Casablanca baada yakuondoshwa kwa mikwaju ya penati 4-3.

Dakika 90 za mchezo zilimalizika kwa Simba kufungwa bao moja bila na hivyo kuwa sare ya bao moja kwa moja katika michezo yote miwili na hivyo kupelekea mchezo huo kwenda katika hatua ya matuta. Wydad walipata penati zao zote nne wakati Simba walikosa penati mbili, Shomary Kapombe na Clatous Chama ndio waliokosa mikwaju ya penati.

Baada ya mchezo kumalizika na Simba kutolewa Chama alisema “Imekuwa ni safari ndefu yenye mambo mengi ndani yake na hisia mchanganyiko. Jana tulifanya kila kitu tunachokijua lakini mwisho wa siku ilibidi tukubaliane na ukweli ili tuweze kusonga mbele. Shukrani za dhati kwa wachezaji, benchi la ufundi, Rais Mo Dewji, na mashabiki.”

Clatous Chama

Mwamba wa Lusaka ambae hakufurukuta kabisa katika mchezo huo licha ya kutegemewa kuonyesha makubwa aliwashukuru mashabiki wa Simba huku wakiyachukulia matokeo yale kama chachu yakusonga mbele.

Clatous Chama “Maombi na upendo wenu ndio umetufikisha hapa leo. Tutachukulia matokeo ya jana kama chachu ya kuendelea kuimarika. Asanteni kwa ushauri na message zenu za kutia moyo. Mungu awabariki sana,”

Simba sasa wameendeleza rekodi yao yakucheza robo fainali pasi na kuvuka kwenda nusu fainali huku hii ikiwa ni mara ya nne ndani ya miaka sita wakicheza robo fainali na kuondoshwa. Awali walitolewa na TP Mazembe mwaka 2019, wakatolewa na Kazier Chiefs mwaka 2021 na mwaka 2022 waliondoshwa na Orlando Pirates katika Shirikisho Afrika.

Sambaza....