Kiungo wa Simba Clatous Chota Chama mpaka sasa amefanikiwa kuweka rekodi ya aina yake katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoendelea ikiwa imebakiza mchezo mmoja kumalizika kwa hatua ya makundi.
Clatous Chama “Mwamba wa Lusaka” aliyeiongoza Simba kufuzu hatua ya robo fainali kwa kufanikiwa kuipa ushindi mara mbili mfululizo Simba dhidi ya Vipers aliyoifunga bao moja na Horoya aliowafunga mabao matatu ndie kinara wa kuhusika na mabao katika michuano hiyo.
Baada ya kufunga mabao matatu katika mchezo dhidi Horoya na kutoa pasi moja ya bao katika ushindi wa mabao saba bila dhidi ya Horoya sasa Chama ndio mchezaji aliyehusika katika mabao mengi zaidi akiwa na mabao manne na pasi moja ya bao.
Katika orodha hiyo ya wachezaji waliohusika na mabao mengi nyuma ya Chama yupo Makabi Lilepo wa Al Hilal katika nafasi ya pili mwenye mabao manne huku nafasi ya tatu ikishikwa na Hamza Khaba wa Raja Casablanca mwenye mabao matatu na pasi moja ya bao hivyo kuhusika katika mabao manne ya timu yake sambamba na mlinzi wa Al Ahly Ali Maaloul mwenye pasi nne za mabao na Casias Mailula wa Mamelodi Sundows mwenye mabao matatu na pasi moja ya bao.
Ushindi walioupata Simba wa mabao saba bila dhidi ya Horoya umewafanya kuwa timu ya nne yenye mabao mengi mpaka sasa wakiwa na mabao tisa nyuma ya vinara Raja Casablanca (14), Mamelody Sundows (12) na Al Ahly wenye mabao 11.
Simba pia imeingia katika rekodi mbovu ya nidhamu kwani mpaka sasa katika michezo mitano wachezaji wake wameonyshwa kadi 12 za njano na wakiwa sawa na Esperance de Tunis ya Tunisia.