Tayari mshambuliaji raia wa Congo DR Fiston Mayele amejiunga na Pyramids ya nchini Misri na kuachana na Yanga aliyodumu kwa miaka miwili yenye mafanikio.
Mayele ambae ametambulishwa na matajiri hao wa nchini Misri siku mbili zilizopita anahitimisha miaka yake miwili ya mafanikio akiwa Tanzania akiitumikia Yanga baada ya kuibuka mfungaji bora mara moja na mchezo bora wa Ligi pia.
Kupitia ukurasa wao rasmi wa klabu Pyramids walimtambulisha Mayele kwa kuandika “Chui kutoka Congo hatimae amewasili Cairo, karibu mshambuliaji wetu mpya.”
Kufuatia kuondoka Fiston Mayele kiungo fundi wa Simba Clatous Chama ametoa maoni yake kufuatia uhamisho wa nyota huyo wa Yanga “Kwa Mayele, ninamfahamu kama mchezaji, najua ni bora. Nadhani ni hasara kwa timu, na ni hasara kwa ligi,” Chama aliambia aliiambia tovuti ya FAR Post ya Afrika Kusini na kuongeza,
“Lakini kama nilivyosema, katika soka, tunahitaji kukua, hivyo kama ameondoka, anafikiri huo ni uamuzi sahihi kwa kazi yake na familia yake. Kwa hiyo, ninaweza kumtakia kila la kheri huko aendako. Natumai atapata muda wa kutosha wa kucheza kama alivyokuwa Yanga.”
Kuondoka kwa Fiston Mayele ni muendelezo wa wachezaji wakigeni wanaochezea Simba na Yanga ambao wamekua wakizitumia klabu hizi mbili vizuri kama daraja lakwenda vilabu tajiri zaidi hapa Afrika. Si tu Mayele kwani hata Clatous Chama, Luis Miquissone na Tuisilia Kisinda walipitia vilabu hivi kwa nyakati tofoauti na kuelekea vilabu vya Uarabuni.