Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Simba Clatous Chama amempokea kwa furaha nyota mwenzake Luis Miquissone baada ya kurejea tena Simba akitokea Al Ahly.
Akizungumza na tovuti ya FARPost Chama ameonyesha kufurahishwa na urejeo huo ambapo miaka mitatu nyuma wawili hao waliunda safu hatari ya kiungo cha Simba.
“Najisikia vizuri kwamba amerudi (Luis Miquissone). Ni jambo zuri kwa klabu na ni jambo zuri kwake kwa sababu, katika miaka michache iliyopita, amekuwa hachezi sana,” alisema Chama na kuongeza
“Al Ahly ni klabu kubwa, na wakati wowote mchezaji mzuri anapokwenda kwenye klabu, ana matumaini ya kupata muda wa kucheza. Natumai atafanya kazi kwa bidii na kurejea kwenye kiwango chake akiwa Simba.”
“Ni nyongeza, yeye ni bora, ni mzuri. Anajua jambo moja au mawili kuhusu ligi ya Tanzania, anajua kinachotakiwa, na anafahamu presha kutoka kwa mashabiki na uongozi.”
Wawili hao Clatous Chama na Luis Miquissone waliondoka kwa pamoja mwaka 2022 ambapo walielekea RS Berkane na Al Ahly lakini sasa wawili hao wote wamerejea Simba ambapo walipata umaarufu na kuonekana baada ya kufanya vyema katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Urejeo wake kwasasa hautokua rahisi kwa Luis kwani katika nafasi yake kuna wachezaji waliofanya vyema msimu uliopita lakini pia hata wapya waliosajiliwa hivyo anahitaji kupambania nafasi yake. Katika eneo lake sasa kuna Kibu Denis, Aubirn Kramo, Essomba Onana na Saidoo Ntibazonkiza.