Wananchi Yanga kesho jioni atakua ugenini akikaribishwa na Wekundu wa Msimbazi Simba katika mchezo wa Ligi ya NBC katika Dimba la Benjamin Mkapa na kuelekea mchezo huo kocha msaidizi wa Yanga ametema cheche akiongea na waandishi wa habari.
Kuelekea mchezo huo Cedric Kaze ambae aliongea kwa niaba ya kocha mkuu Nasradinne Nabi amesema anajua wanakwenda kucheza mchezo mkubwa Afrika tena mbele ya mashabiki wengi lakini wamejiandaa kwa hilo na wamendaa wachezaji wao vizuri.
Cedrick Kaze “Tumejiandaa vizuri na kwa utulivu mkubwa, tunajua kesho tunakwenda kwenye moja kati ya michezo mikubwa Afrika na sio kila mara tunacheza mechi inakua na mashabiki elfu hamsini ni lazima twende na tuwatendee haki mashabiki na tumejiandaa vizuri kwa hilo.”
Katika hatua nyingine pia Cedrik Kaze amesema timu yake ina wachezaji bora na wakubwa na ndio maana wao ni bora. Kaze amezungumza kwamba wachezaji wakubwa ndio huamua mechi kubwa na kuipa timu makombe.
“Mechi kubwa huamuliwa na wachezaji wakubwa lakini makombe yanabebwa na timu kubwa yenye wachezaji wakubwa na kikosi bora,” alisema Kaze
Yanga katika mchezo wa awali waliambulia sare mbele ya Simba ambapo iliwalazimu kusawazisha kupitia Aziz Ki baada ya bao la mapema la Augustine Okrah na hivyo mchezo kumalizika kwa sare ya bao moja kwa moja.