Michuano ya wanawake kwa nchi wanachama wa Baraza la vyama vya michezo ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Women Championship) iliyotakiwa kufanyika kuanzia Mei 12 hadi Mei 22 mwaka huu yameahirishwa.
Katika taarifa iliyotolewa na Shirikisho la soka la Rwanda (FERWAFA) imeeleza kuwa sababu kubwa ya kuahirishwa tena kwa mashindano hayo ambayo awali yalitakiwa kufanyika mwezi Novemba hadi Disemba mwaka jana ni kutokana na kukosekana kwa fedha.
“Sababu kubwa ya kuahirishwa kwa mashindano ni kutokana na kukosekana kwa fedha kwa nchi mwenyeji (Rwanda) ambayo awali ilipaswa kutumwa kwetu (FERWAFA) na CECAFA” Ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Tayari vikosi vya timu za soka za Rwanda, Kenya, Uganda, Zanzibar, Tanzania Bara, Ethiopia na Djibouti vilikuwa katika maandalizi kujiandaa na michuano hiyo ambayo mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2016 nchini Uganda na Tanzania Bara kufanikiwa kutwaa taji kwa kuichapa Kenya kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali.