Aliyekua mshambuliaji wa klabu ya Chelsea Tony Cascarino ameonesha kuchukizwa na mfumo wa meneja wa sasa wa klabu hiyo Maurizio Sarri, kwa kusema haumpi nafasi kiungo kutoka nchini Ufaransa N’Golo Kante, kucheza kama ilivyokua misimu miwili iliyopita.
Cascarino ambaye aliitumikia Chelsea kuanzia mwaka 1992–1994 na kufunga mabao manane katika michezo 40, amesema Sarri anahisi anampa uhuru Kante, lakini jambo hilo hadhani kama lina nafasi kwenye moyo wa kiungo huyo, ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichotwaa ubingwa wa dunia mwaka huu.
Amesema Kante alionesha kuwa mzuri na msaada mkubwa kwenye kikosi cha Chelsea kwa misimu miwili, kutokana na nafasi aliyokua akiachiwa kucheza kama kiungo mkabaji wakati wote, lakini tangu alipofika meneja Sarri klabu hapo, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27, amekua akihangaika uwanja mzima.
“N’Golo Kante anaonekana hana furaha kutokana na nafasi anayochezeshwa tangu Sarri alipoingia Chelsea,” Cascarino aliliambia gazeti la The Times.
“Ninahofia hali hii inaweza ikawa janga kwa Chelsea katika michezo ya baadae, maana ukiwa na mchezaji ambaye hafurahii utumishi wake kikosini, lolote linaweza kutokea.”
“Kante alipaswa kupewa heshima yake kama ilivyokua misimu iliyopita, alionesha kiwango kizuri na aliisaidia sana timu, ninashangazwa na hili tunaloliona kwa sasa, kuna haja meneja akafanya mabadilio haraka iwezekanavyo, la sivyo ninahofia mambo kuwa magumu kwa baadae.”
“Bado anaonekana ana uwezo mkubwa wa kupambana, lakini anavyochezeshwa sasa ni sawa na kumchosha mapema, kuzunguuka uwanja wote kusaidia kukaba, sio kazi ndogo,”
“Sioni sababu ya kumtumia Jorginho kama kiungo mkabaji wakati wote, ingependeza watu hawa wawili wakasiadiana majukumu.”