Zanzibar ndipo kitovu chake kilipozikwa, kitovu ambacho kilikuwa na siri kubwa, siri ambayo ilikuwa inaonesha kuwa kuna mwanasoka imara kazaliwa katika ardhi hiyo.
Mwanasoka ambaye mpaka anamaliza maisha yake ya soka kafanya dhambi moja tu nayo ni dhambiya kutocheza soka la kulipwa.
Alikuwa na vigezo vingi ambavyo vingemwezesha kuwa mchezaji wa kulipwa kama walivyo kina Mbwana Samatta, lakini kwa bahati mbaya Nadir Haroub “Cannavaro” alichagua dini ya kutokuwa na wasimamizi bora wa kipaji chake.
Huu ndiyo huwa ni mwanzo wa wachezaji wengi kutonufaika na vipaji vyao. Wengi wao wameamua kuchagua dini ya kutokuwa na wasimamizi bora wa vipaji vyao.
Hiki ndicho kilichomfanya Nadir Haroub “Cannavaro” kumaliza muda wake wa kucheza soka la ushindani akiwa na jezi ya Yanga.
Hajawahi kuivua jezi hii tangu miguu yake ikanyage Jangwani. Miguu yake ilipenda udongo wa Jangwani, hali ambayo ilisababisha akili yake kutofikiria sana kutoka katika ardhi hii ya Tanzania.
Ardhi ambayo ilimfanya Samuel Eto’o kumfuata Nadir Haroub “Cannavaro” kwa ajili ya kuomba jezi yake baada ya mchezo kati Tanzania na Cameroon kumalizika.
Hii ilikuwa ishara tosha kuwa Nadir Haroub “Cannavaro” alikuwa na kipaji kikubwa , kipaji ambacho kilimjengea heshima mpaka kwa Samuel Eto’o.
Hii inatosha kuonesha kuwa Nadir Haroub “Cannavaro” anastaafu mpira akiwa hajatimiza kitu ambacho alitakiwa kukitimiza.
Lakini kwa bahati mbaya leo hii hana uwezo tena wa kucheza soka la ushindani kwa hali ya juu.
Miguu yake haina nguvu tena ya kupambana na Samuel Eto’o. Hana kasi ya kukimbizana na Samuel Eto’o kwa kifupi siku zake zimefika ukingoni.
Alichobakiza na kuishi maisha mengine nje ya uchezaji. Inawezekana busara zake zinaweza kutumika kwenye benchi la ufundi.
Na kuna uwezekano mkubwa akawa kocha bora kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusoma mchezo na kuna uwezekano maisha haya yanaweza kumtendea haki kuliko maisha ya uchezaji.
Leo hii tunapomwandika kama mchezaji mstaafu tunatakiwa tutafakari ni wachezaji wangapi wenye vipaji vikubwa ambao humaliza maisha yao ya soka wakiwa hapa nchini?
Ni wachezaji wangapi wanamaliza maisha yao ya mpira wakiwa masikini kutokana na kutumia muda mrefu wakizitumikia vilabu vyetu masikini?
Ni wachezaji wangapi ambao hawana wasimamizi bora wa vipaji vyao?, wasimamizi ambao wanauwezo wa kutafuta mazingira bora ya mchezaji. Mazingira ambayo yatamwezesha mchezaji apate timu ambayo itakuwa na manufaa makubwa kuanzia kwenye kipaji chake cha kucheza mpira mpaka kwenye uchumi.
Tupo kwenye dunia ambayo mpira ni biashara, ile dunia ya kusema mpira ni sehemu ya furaha na kujenga afya wakati wake umeshapita.
Leo hii wengi wa wachezaji wanafikiria namna ambavyo wanaweza kuingiza pesa kupitia vipaji vyao vilivyowekwa miguuni.
Leo hii Nadir Haroub “Cannavaro” alitakiwa kumaliza mpira akiwa kama balozi wa kampuni yoyote ya biashara lakini kwa sababu hakuwa na wasimamizi bora wa kipaji chake leo hii anamaliza safari yake akiwa mkiwa.
Pamoja na kwamba bado ana nafasi ya kulitumia jina lake, lakini ilikuwa busara kwake yeye kunywa supu wakati ikiwa ya moto.
Wakati miguu yake ilipokuwa na nguvu ndiyo ulikuwa wakati wa yeye kutengeneza pesa.
Wengi wa wachezaji wetu wanamtazama Nadir Haroub “Cannavaro” kama mchezaji imara, mwenye busara kubwa ndani ya uwanja na kwenye vyumba vya kubadilishia nguo lakini hawataki kutazama upande wa pili wa Nadir Haroub “Cannavaro”.
Upande ambao ndiyo kuna mengi ya kujifunza kwenye dunia hii ya kibiashara.
Dunia ambayo mchezaji kuwa bila na wasimamizi bora wa vipaji vyao ni sawa na kujiingiza kwenye tanuru la moto wa umasikini.