Timu ya wataalamu kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ipo nchini kukagua miundombinu ya michezo ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027 endapo nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zitapata ridhaa ya kuandaa mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Akifungua kikao cha kuwakaribisha wataalam hao, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali ya Tanzania ipo tayari kuandaa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda kwa kuwa Tanzania uamuzi huo umefanyiwa kazi katika ngazi ya juu ya serikali.
“Mimi binafsi niliwasilisha Ajenda hii katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wote na ilipitishwa kwa kauli moja na maagizo yakatolewa kwamba tuendelee na taratibu za kuandaa mashindano haya” amesema Balozi Dkt. Chana.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Saidi Yakubu amesema tayari Serikali imesaini mkataba wa makubaliano ya ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) ya China ambao utagharimu Sh. Bilioni 31, ili kufanikisha azma hiyo ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ambazo ni sehemu ya Umoja wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki ambazo zitaandaa kwa mara ya kwanza mashindano ya AFCON tangu mashindano hayo yaanzishwe.
Katibu Mkuu Bw. Yakubu ametaja maeneo ambayo yatafanyiwa ukarabati kuwa ni eneo la vyumba vya wachezaji, chumba cha waandishi wa Habari, eneo la watu mashuhuri (VVIP), kubadilisha viti vyote vya kukalia mashabiki uwanjani hapo, ubao wa kuonesha matokeo, kuweka mfumo mpya wa TEHAMA, kubadilisha eneo la kuchezea na seti mbili za magoli ambazo zitatumika uwanjani hapo.
Maeneo mengine ambayo yatafanyiwa ukarabati ni viti vya benchi la ufundi na wachezaji wa akiba, mfumo wa umeme, mfumo wa sauti, eneo la kukimbilia wanariadha, chumba cha VAR, lifti mbili mpya, mfumo wa taa, mfumo wa maji taka, mgahawa pamoja na vitu vingine ambavyo vimepita muda wa matumizi kwani vilitakiwa kutumika kwa muda wa miaka saba tu.
Ukaguzi huo umehusisha Uwanja wa Benjamin Mkapa, Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. Julius Julius Nyerere, hospitali ya Taifa Muhimbili, Uwanja wa Uhuru, na viwanja vingine vya mazoezi.
Kwa upande wake Mkuu wa Msafara Omar El Ghiathi amesema katika ziara yao ya ukaguzi wamefurahishwa na utayari wa nchi hizo tatu ambazo zimeungana kuomba kupewa ridhaa na CAF kwa kauli yao ya Pamoja Bid ili kuandaa mashindano ya AFCON 2027.