KOCHA mkuu wa Simba SC, Patrick Aussems raia wa Ubelgiji bila shaka ana kikosi kipana, lakimni kuanzia leo Jumamosi naweza kuanza kuona presha kubwa ikielekezwa kwake. Atapata presha kutoka kwa wachezaji wake watatu wa nafasi ya ushambuliaji. Nahodha, John Bocco, mfungaji bora wa msimu uliopita Mganda, Emmanuel Okwi na kinara mpya wa mashambulizi na ufungaji klabuni hapo Mnyarwanda, Meddie Kagere.
Si hivyo tu, Aussems ataanza kupata presha ya mashabiki na pale kikosi chake kitakapoendelea kutofunga magoli ya kutosha atanyoshewa vidole na watu kuanza kuhoji uwezo wake kiufundishaji. Nani atakayekuwa pacha wa Kagere, na nani atakayekubali kuhamia upande wa pembeni ili kucheza pamoja katika safu ya washambuliaji watatu?
NI LAZIMA MMOJA ASUBIRI BENCHI…..
Okwi alifunga jumla ya magoli 20 na kushinda tuzo ya mfungaji bora wa ligi kuu msimu uliopita, Bocco alifunga magoli 14 na kumaliza katika tatu bora na huku mfungaji bora namba mbili wa ligi msimu uliopita, Marcel Kaheza naye akijumuika katika kundi la washambuliaji wa Simba msimu huu, na Mohamed Rashid aliyefunga goli 12 akiwa Prisons
Inamaanisha ‘Wekundu wa Msimbazi’ wamewakusanya washambuliaji wote wane bora katika ligi ya msimu uliopita. Kagere ambaye alikuwa na mafanikio Gor Mahia FC katika ligi kuu ya Kenya, licha ya kutofanikiwa kutwaa tuzo yoyote ya ufungaji bora katika misimu yake mitatu KPL, raia huyo wa Rwanda ni chaguo ambalo linamfanya Aussems kumtazama kama-namba moja.
kuwa na wafungaji wote hawa watano ni mzigo kwa kocha hasa ukizingatia timu ina viungo washambuliaji-wafungaji wengine kama Mohamed Ibrahim, Muzamiru Yassin na Adam Salamba. Kama kocha, Aussems atakubali shinikizo, atapaswa kutumia mfumo wa 4-3-3 ili kuwapanga kwa wakati mmoja Kagere aliyekwishafunga magoli matatu katika michezo miwili ya mwanzo, Bocco na Okwi.
Kumuacha nje yeyote kati yao ni changamoto kubwa sana kwa kocha yoyote na hapa ndipo Aussems anapaswa kuwajenga vizuri kisaikolojia mastraika wake hao-viongozi watatu. Kwa Kaheza, Mohamed na Salamba hakuna tatizo hata kama wataachwa nje, lakini si rahisi kwa kocha huyo kupata mafanikio kama hatawaambia mapema Okwi, Kagere na Bocco kwamba watapaswa kucheza mara nyingi zaidi kwa kubadilishana nafasi, huku akiwatumia pamoja katika michezo baadhi.
Kumuweka yeyote benchi bila kuzungumza nao kwa pamoja itaanza misuguano kwa sababu wowte, Bocco, Okwi na Kagere watataka kuongoza mashambulizi, huku kundi la Kaheza, Mohamed na Salamba likijengwa zaidi kama wasaidizi wa washambuliaji hao watatu mastaa. Kuzungumza nao kabla ya kuanza kuwatumia ni vizuri kuliko kocha kufanya maamuzi kwa kutazama tu uwezo wa mchezaji uwanjani.
Kati ya Bocco na Okwi mmojawapo atapaswa kumpisha Kagere ili kuifanya timu icheze kwa balansi katika ulinzi, kiungo na mashambulizi. Je, ni nani atakayempisha? Wote wanaweza kucheza vizuri katika mfumo wa washambuliaji wawili pacha-labda, 5-3-2 ama 4-4-2, Okwi anaweza kumuongezea mwanya kocha Aussems kwa sababu anaweza kucheza kulia katika wing ama kusho.
Okwi ana fiti katika 4-4-2 na 4-3-3 pia lakini kama atapelekwa pembeni inamaanisha kuna wachezaji kama Mzambia, Chama, Hassan Dilunga na Mnyarwana Haruna Niyonzima watakosa nafasi. Je, Erasto Nyoni atarudi katika beki?
Kama Nyoni atabaki katika kiungo itakuwa vizuri zaidi kwa sabnabu ndiye mchezaji anayeanzisha vizuri mashambulizi na ulinzi wake ni salama zaidi, lakini bado Aussems anaweza kuamua mwenyewe mifumo na vikosi vyake lakini vitaongozwa na maamuzi atakayofanya kuhusu Bocco, Okwi na Kagere. Je, awachezeshe pamoja? Na je timu itakuwa katika uwasa wakicheza pamoja?, kama sivyo nani wa kumuweka nje? Atakubali?
Jonas Mkude, Mghana, James Kotei, Niyonzima, Shiza Kichuya, Chama, Dilunga nao kuanza kwao kikosi cha kwanza kunategemea zaidi maamuzi ya kocha Aussems kuhusu kuwapanga pamoja ama kumpanga mmoja au kuwapanga wawili, Bocco + Kagere; Kagere + Okwi, Bocco + Okwi na si Kagere + Bocco + Okwi, timu itakosa balansi, na mmoja akikaa nje na magoli yakikosekana pia itakuwa tatizo hapo ndipo napoanza kuamini Aussems ataanza kuingia katika presha hasa leo Jumamosi watakapokuwa wageni wa Ndanda FC katika uwanja wa Nang’wanda, Mtwara.