Nikikumbuka kuwa ndiye mchezaji wakwanza kufikisha mabao 100, kwenye Ligi Kuu Tanzania tangu kumbukumbu zianze kutunzwa vyema, basi nakosa la kuandika.
Hiyo tayari ni mada ndefu yenye mengi ndani yake, itoshe kumheshimu na kumpongeza mfumania nyavu huyo aliyefunzwa Azam akaja kufundisha Simba.
Mwaka 2008 alivaa rasmi Jezi nyeupe na bluu za waoka mikate wa Chamazi Azam Fc na kuanza kula kitabu cha soka kwa vitendo zaidi katika Ligi Kuu Bara.
Alikua kijana mmoja mpole mwenye uwezo mkubwa, goli aliliona kila alipopata nafasi, wakati wachezaji wengi wakitaka kwenda vilabu vikubwa na hata nje ya nchi yeye alitulia na kuamini kua Azam ni shule tosha kwake.
Ilifika muda akapewa usinga, akawa kiongozi wa vijana wa mzee Bakhresa uwanjani na April 2014 akawaongoza wanalambalamba hao kubeba ubingwa wa Ligi Kuu na kuvunja mwiko wa Simba na Yanga pekee ndio mabingwa.
Mwaka 2017 nyasi za Chamazi Complex zilivuja jasho la huzuni ‘umande’. Mashabiki wale wa Vigoma mikono iliachia ngoma na kushika mashavu hayo yote ni baada ya kusikia kuwa yule kinara wao wa mabao John Raphael Bocco Amehitimi mafunzo yaliyo muweka Chamazi pale kwa zaidi ya miaka 10, na inambidi akatafute maisha mengine, ilikuwa huzuni sana mitaa ile.
Akamwaga wino Simba Sc, Msimbazi wakachekelea, muda mchache mazoezini Jonas Mkude akavua kitambaa akamkabidhi burudani ikaanza, akaanza kutoa shule kwa Washambuliaji Simba na Bongo kwa ujumla.
Mabeki na makipa wengi ukiwauliza mshambuliaji gani wanamuogopa kuliko watamtaja Bocco, pande la mtu futi sita kwenda juu, utamwambia nini?.
Washambuliaji walio wengi ndoto zao ni kuwa kama mkufunzi huyu, mashine ya mabao, hakika elimu anaitoa vyema. Nidhamu, uwajibikaji na kujituma ni Elimu nyingine kubwa anayoitoa Bocco kwa wachezaji wa Bongo, anafundisha kwa vitendo.
Mungu ni wetu sote, imani ni kubwa kuwa ataendelea kuihudumia Simba na Taifa kwa ujumla na baadae ataondoka zake kupumzika na kuacha Historia watakayoisoma wanetu na wajukuu pia.