Benki ya CRDB imetangaza kuanza rasmi kwa kampeni ijulikanayo kama “Furahia kandanda murua nchini Urusi” #TwenzetuRussia, itakayowawezesha watumiaji wa kadi za malipo za TemboCard Visa za Benki hiyo kujishindia safari ya kwenda kuangalia mechi za michuano ya kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Urusi, kuanzia mwezi Juni mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa Benki hiyo Bi. Tully Esther Mwambapa, alisema kuwa Benki ya CRDB imeanzisha kampeni kwa kushirikiana na kampuni ya Visa International ili kutoa fursa kwa wateja wake kwenda kushuhudia fainali hizo, ambazo huvutia hisia za watu wengi dunuani kote. “Wateja wetu wenye TemboCardVisa, TemboCardVisa-Electron, TemboCard Visa-Gold, TemboCardVisa-Platinum na TemboCardVisa-Infinite, wakati wa kampeni hii watatakiwa kulipia bidhaa au huduma wanazonunua kwa kutumia TemboCardVisa zao kupitia mashine za malipo (POS) zilizopo sehemu mbalimbali kama kwenye migahawa, maduka, mahospitali, vituo vya mafuta na kwingineko, ili waweze kujishindia zawadi hii kubwa” alisema.
Bi.Mwambapa aliendelea kusema kuwa “iii mteja aweze kushinda, anatakiwa kufanya miamala mingi zaidi kila wiki na kadri mteja anavyolipia zaidi kwa kutumia TemboCardVisa yake, ndivyo anavyojiongezea nafasi kubwa zaidi ya kushinda. Washindi wa wawili watakaokuwa wamefanya miamala mingi zaidi kila wiki watajishindia safari ya kwenda Urusi ambayo itagharamiwa kila kitu na Benki ya CRDB, ambapo jumla ya tiketi 24 zitatolewa” alisema Bi. Tully Mwambapa.
Bi.Mwambapa aliendelea kusema kuwa pamoja na washindi wawili wa kwanza kujishindia safari hiyo, Benki pia kila wiki itatangaza washindi wengine 10 kupitia vyombo mbalimbali vya habari ambao watajishindia zawadi kemkem ikiwemo luninga zitakazokuwa zimeunganishwa na kulipiwa kinga’muzi cha DSTV, jezi za timu za mataifa mbalimbali, mipira, kofia, fulana na na zawadi zingine nyingi.
Maelezo zaidi kuhusu kampeni hii:
- Ni lazima kuwa mteja mwenye akaunti ya Benki ya CRDB
- Ni kwa wateja wenye kutumia Kadi ya TemboCard Visa za Benki ya CRDB
- Ili kushinda unatakiwa kufanya manunuzi na malipo mengi zaidi kupitia mashine yoyote ya POS zilizopo katika vituo tofauti nchini (Petrol station, Supermarket, Hotels, National Parks, Hospitals na zingine nyingi)
- Manunuzi/malipo yafanyike kupitia POS yoyote na si lazima iwe ya benki ya CRDB
- Manunuzi na matumizi yanaweza pia kufanyika nje ya nchi
- Washindi watakuwa ni wale wenye miamala mingi ya TemboCard Visa kila mwisho wa wiki na watapatikana kupitia “draw” maalumu
- Washindi 10 zaidi watazawadiwa kila wiki
- Benki itagharamia safari nzima ikiwemo usafiri, malazi na kujikimu
- Jumla ya tiketi 24 za mechi mbalimbali ikiwemo tiketi 4 za mechi za nusu fainali kutolewa
Kuhusu Benki ya CRDB
Benki ya CRDB ilianzishwa mwaka 1996 na imeendelea kukua zaidi hadi kufikia kuwa benki inayoaminika, chaguo la kwanza la mteja na kuongoza kwa ubanifu katika soko. Benki ya CRDB imekuwa ikirekodi ongezeko la faida kila mwaka tokea ilipoanzishwa na imekuwa ikilipa gawio kila mwaka kwa wanahisa wake. Benki ilipiga hatua muhimu hivi karibuni baada ya kuvuka mipaka ya Tanzania na kuanzisha kampuni tanzu ya CDRB Burundi.
Benki ya CRDB inatoa huduma mbalimbali kwa wateja wakubwa, wakati na wadogo kupitia matawi zaidi ya 250, Matawi yanayo tembea 13, Mashine za kutolea fedha zaidi ya 515, vifaa vya manunuzi (PoS) zaidi ya 1,000 na Mawakala wa FahariHuduma 2,558. Pia Benki ya CDRB inatoa huduma ya kibenki kupitia mtandao yaani “Internet banking” na huduma ya kibenki kupitia simu ya mkononi ijulikanayo kama “SimBanking”.