Beki wa pembeni wa Stand United Miraji Makka amekanusha tetesi za kuhusishwa kujiunga na timu za Azam na Yanga na kusema kwamba mpaka sasa hakuna timu yoyote kati ya hizo ambazo zimemfuata kutaka kuzungumza naye.
Akizungumza na mtandao huu akiwa anajiandaa kwa ajili ya kucheza na Ndanda katika mchezo wa mwisho wa Ligi msimu huu, Makka amesema japokuwa mkataba wake na Stand United umekwisha lakini angependa kuona akiendelea kukipiga katika timu hiyo msimu ujao na anasubiri mazungumzo ya kimkataba lakini amesema hazuii timu nyingine kuzungumza naye.
“Kusema ukweli hakuna viongozi wa Azam wala Yanga ambao wamenifuata kuzungumza na mimi, ni tetesi tu na sijakataa kuzungumza nao, nimesikia baadhi ya watu wakisema tayari nimeshamalizana na Azam lakini hilo si la kweli, na hakuna asiyependa kucheza timu kubwa kama Yanga wakija na ofa nzuri nipo tayari kujiunga nao, ila kwa sasa wacha ligi iishe kwani bado nina matumaini ya kubaki hapa Stand United,” Makka amesema.
Makka ambaye aliwahi kuichezea Toto Africans ya Mwanza, amekuwa na msimu mzuri akicheza kama beki wa kushoto katika timu ya Stand licha ya mwanzoni kukosa michezo michache kutokana na kuwa na majeraha.
Awali taarifa zilieleza kwamba Salim Hoza ambaye alikuwa naye Toto Africans ndiye aliyemshawishi kujiunga naye Azam na kwanza tayari mazungumzo ya kujiunga na timu hiyo ya wahoka mikate ilikuwa ikifanyika ili ajiunge nao pamoja na beki wa kati ambaye ni Ally Ally.