HAYIMAYE uvumi umekuwa kweli. Chelsea imepangwa na Barcelona hatua ya 16 ya Uefa Champions league. Ilianza kama uvumi, ikaja tetesi, lakini mchana wa leo viganja vya Xabi Alonso vimefanya ndoto ya wengi iwe kweli.
Ni mechi ya kiume. Ni mechi ya kigumu. Ni mechi inayokutoa machozi, jasho na damu kwa wakati mmoja. Hii ni fainali iliyotangulia kabla ya fainali yenyewe iliyopangwa kupigwa nchini Ukraine kwenye jiji la Kyiv.
Dakika chache ya Alonso kushika kile kikaratasi kilichoonyesha Chelsea itacheza dhidi ya Barcelona, simu za mashabiki wa timu nyingine ziliita kwa fujo kwenye simu yangu ya kiganjani. Hakuna hata simu moja niliyoipokea. Najua walikuwa wanataka kuniambia nini na mimi nimeamua kuja na andiko hili kama majibu ya walichotaka kuniambia na kuwafahamisha tabia za Chelsea kwenye mechi za namna hii.
Niwaambie tu Chelsea haijawahi kuwa na hofu na michezo kama hii. Na hii ndiyo michezo inayoonyesha uimara wetu na umwamba wa ulaya. Hivi nani amesahau tukio la Didier Tito Drogba Munyama, Mei 25, 2012 pale Arianz Arena alipoganda hwani dakika kadhaa na kupiga ‘shuti’ la kichwa lililoenda moja kwa moja kwenye nyavu za Manuel Neuer? Nadhani tunakwenda sambamba.
Wiki iliyopita Hazard alisema Chelsea haina hofu ya kupangwa na yeyote yule katika hatua hii, unadhani nani mwingine anayeweza kusimama juu ya kauli hii na kuipuuza kirahisi? Hapa Hazard alisimamia kile tunachokiamini sisi mashabiki wa Chelsea.
Kama kauli ya Hazard ingezungumzwa na mchezaji mwingine nje ya Chelsea ningejawa na mashaka iliyokolezwa na hofu ndani yake, lakini kwa kuizungumza Hazard tunajiona tayari tuko mguu mmoja ndani ya Kyiv tukisubili timu ya kupambana nayo.
Wakati mwingine mechi za namna hii, zinatakiwa kwenda sambamba na kauli za kishujaa kama hizi. Unadhani Barcelona wameifurahia hii ratiba haswa wakikumbuka kilichowatokea Stamford Bridge kwa Drogba kufunga bao 1-0, huku Torres akienda kuwazima nyumbani kwao? Hawajaifurahia!
Namba hazidanganyi. Chelsea ndiyo timu pekee inayoinyanyasa Barcelona mara nyingi walipokutana kuliko timu nyingine ndani ya Uingereza. Kuna timu ya Uingereza mashabiki wake wananuna na kuchukia wakipangiwa Barcelona. Chelsea ndiyo timu pekee kutoka Uingereza ambayo ikipangwa na Barcelona mashabiki wake tunashangilia na hatuna tone la hofu. Wanatujua vizuri tukiwa kwenye hatua kama hii.
Kando ya Chelsea nawapenda sana Barcelona na staa wao Messi. Lakini kwa sasa waniache kidogo. Wameshageuka maadui wetu, sina sababu ya kuwashangilia tena mpaka mechi yetu iishe.
Kuna mengi yaliyonifanya niipende Chelsea na kuichukia Barcelona kwa sasa. Chelsea imevunja tawala za timu nyingi kubwa Uingereza. Chelsea imetufungulia dunia kuwa tunachokitaka. Naanzaje kuichukia timu hii?
Barcelona hii iko hovyo sana. Haivutii tena wala haichezi vizuri. Kama tuliweza kuwatoa nishai wakati ule waliokuwa na Ronaldinho Gaucho, Samuel Etoo, Xavi Hernandez, Andres Iniesta na Puyol, tunakuwaje na hofu kwa Barcelona hii ya Dembele, Delofour, Semedo na Jordi Alba? Waleteni hao Barcelona wenu.
Umapokuwa na Hazard, Morata, Kante, hautakiwi kuwa na hofu na yeyote yule zaidi ya mungu. Chelsea tuna hofu na mungu sio Barcelona au timu nyingine. Ikiwezekana tukiwatoa hawa Barcelona tupeni timu nyingine ngumu ngumu.
Anyway natazama marudio ya Chelsea msimu wa 2011/ 2012 iliposhinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa anayehitaji kutazama aje inbox nimtumie link naye aione nguvu ya Chelsea inapokuwa maeneo nyeti kama haya.