Sambaza....

Baada ya mechi kati ya Simba na Al Alhy moja ya vitu ambavyo nilikuwa naviangalia sana ni ratiba ya Simba katika michuano ya ligi kuu.

Ratiba ambayo ilikuwa inamtaka acheze mechi moja kila baada ya siku tatu. Kiuhalisi hiki ni kitu kigumu sana kwa kocha na wachezaji kwa ujumla.

Mechi moja ndani ya siku tatu ? , tena kwenye nchi ambayo miundombinu yake siyo mizuri ukilinganisha na nchi zilizoendelea?

Yani timu itoke Dar, baada ya siku tatu inatakiwa icheze mechi Iringa, baada ya siku tatu inatakiwa icheze mechi Shinyanga.

Itoke Shinyanga, iende Dar tena kucheza mechi. Unacheza ndani ya muda mfupi bila mapumziko kwa wachezaji.

Wachezaji wanatumia muda mrefu kusafiri kutoka sehemu moja au nyingine. Yani uchovu wa mechi, ukajumuisha na uchovu wa kusafiri lazima kama kocha kichwa kikiume.

Maana kuna kuwa na hatari kubwa mbili kwenye timu, moja timu inaweza ikacheza chini ya kiwango kutokana na uchovu.

Pili kunaweza kuwa na uwezekano mkubwa wa wachezaji kupata majeraha kutokana na wao kucheza mfululizo bila kupumzika.

Lakini mpaka sasa hivi kuna kitu ambacho kimeonekana kinaweza kuwasaidia sana Simba kwenye ratiba hii ngumu, nacho ni kikosi kipana.

Baada ya mechi dhidi ya Al Ahly , Simba ilitakiwa kucheza dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa ligi kuu na hii ni baada ya siku tatu kutoka katika mchezo dhidi ya Al Alhly.

Kikosi ambacho kilicheza mechi dhidi ya Al Alhy ndicho hicho ambacho kilicheza dhidi ya Yanga. Kikosi hiki hakikuwa na nguvu sana kwa sababu ya uchovu.

Kadri muda ulivyokuwa unazidi kwenye mechi dhidi ya Yanga kikosi hiki kilikuwa kinapungukiwa nguvu kwa kiasi kikubwa.

Lakini baada ya mechi kati ya Yanga na Simba, Simba walitakiwa kusafiri mpaka Arusha kucheza dhidi ya African Lyon.

Katika kile kikosi kilichocheza hiyo mechi , asilimia kubwa ya wachezaji walifanyiwa mabadiliko. Kulikuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi.

Hapo ndipo likaja swali moja, Simba inaweza kushinda chini ya kikosi ambacho wengi hawakukizoea kukiona kikicheza ?

Lakini mwisho wa Siku Simba walifanikiwa kushinda magoli 3-0 katika mechi hiyo. Walishinda na kikosi tofauti na kile kilichocheza dhidi ya Al Alhy na Yanga.

Walienda Lipuli baada ya hapo, kukafanyika tena mabadiliko ya kikosi kutoka kwenye kikosi ambacho kilicheza mechi dhidi ya African Lyon.

Pamoja na kwamba Simba walifanya mabadiliko ya kikosi walifanikiwa kushinda goli 3-1 ugenini katika uwanja wa Samora dhidi ya Lipuli FC.

Jana walikuwa wanacheza na Stand United ya Shinyanga katika uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.

Hawa ni wababe wa Yanga, ndiyo waliowafunga Yanga baada ya kwenda michezo 15 bila kufungwa. Hivo wengi tulitegemea Simba itapata upinzani mkubwa kama ambao Yanga waliupata baada ya kukanyaga nyasi za CCM Kambarage.

Na Simba walifanya mabadiliko ya kikosi, kutoka kwenye kikosi ambacho kilicheza kwenye uwanja wa Samora dhidi ya Lipuli.

Pamoja na kwamba Simba walifanya mabadiliko ya kikosi kwenye mechi ya Jana, Simba ilifanikiwa kushinda magoli 2-0.

Hii inatoa tafasri tosha kabisa Simba wanakikosi kipana , kikosi ambacho kinawasaidia katika kipindi hiki cha ratiba ngumu kwao.

Sambaza....