Sambaza....

Kuna vitu vingi sana ambavyo vishawahi kuongelewa kuhusu Ibrahim Ajib. Vingi sana!. Vitu vyote hivo ukivitazama vizuri utagundua kitu kimoja, watu wengi wanakipenda kipaji cha Ibrahim Ajib.

Watu wengi wana mapenzi ya dhati dhidi ya kipaji cha Ibrahim Ajib Migomba. Na ndiyo maana wengi hupenda kuongelea sana kuhusu yeye.

Leo akigundulika ni mvivu, watu wengi hupaza sauti kumsihi asiwe mvivu, kesho akigundulika ni mtovu wa nidhamu, midomo ya watu hufunguka kwa kumsihi awe na nidhamu.

Hata anavyoachwa kwenye timu ya taifa, watu wengi hupaza sauti kwa ajili ya kumpigania Ibrahim Ajib Migomba ili tu aitwe ndani ya kikosi cha timu ya taifa.

Na hata kipindi ambacho Simon Msuva na Mbwana Samatta wanavyofanya vizuri kwenye vilabu vyao, watu hupaza sauti zao kwa Ibrahim Ajib Migomba.

Lengo aone wivu na aongeze juhudi ili tu atoke kwenye ligi hii na kwenda kucheza kwenye ligi kubwa kwa sababu tu anakipaji kikubwa ambacho hakistahili kuwepo kwenye ligi yetu.

Kipaji ambacho hakistahili hata kidogo kucheza kwenye nyasi mbovu kama nyasi za viwanja vingi vinavyotumika kwenye ligi kuu.

Ajib (kulia) akiwatoka mabeki wa Simba

Ligi ambayo ina waamuzi wabovu, ligi ambayo hata uendeshaji wake ni mbovu, kuanzia ratiba mpaka kuitangaza ligi kibiashara.

Ndiyo maana tunamaliza ligi bila kuwa na mdhamini yoyote ndani ya ligi kuu. Ligi ambayo vilabu vinakosa hata hela ya mafuta ya gari zinavyokwenda mkoa mwingine kwa ajili ya mechi.

Ligi ambayo vilabu vinakosa mpaka hela ya mishahara kwa wachezaji. Wachezaji wanacheza kimasikini, wachezaji wanacheza kwa kuwakopesha viongozi.

Ndiyo ligi yetu, ligi mbovu ambayo haitamaniki hata kuangaliwa, ndiyo ligi ambayo wengi wetu tulikuwa tunaona miguu ya Ibrahim Ajib Migomba haifai kuchezea hapa.

Ndiyo maana kila uchwao sauti nyingi huwa zinasikika kumhisi Ibrahim Ajib Migomba afikirie kuondoka kwenye ligi yetu hii.

Kwa kifupi watu wengi wamegeuka kuwa washauri wa Ibrahim Ajib, wamegeuka kuwa watetezi wa Ibrahim Ajib kwa sababu tu ya kipaji chake.

Wanaamini katika kipaji chake, ndiyo maana ndoto zao ni kumuona Ibrahim Ajib Migomba akiwa anacheza katika ligi kubwa na yenye ushindani kuzidi ligi yetu.

Wakati wengi wetu tunawaza hivo na kuombea hiki kitu kitokee kwa Ibrahim Ajib Migomba, yeye anawaza tofauti kabisa na mategemeo yetu.

Yeye haoni kama ana sababu ya kwenda kucheza kwenye ligi yenye ubora kuzidi ligi yetu hii. Yeye mpaka sasa hivi hajaona sababu ya kuondoka kwenye ligi yetu.

Huyu ndiye Ibrahim Ajib Migomba ambaye amekataa kujiunga na TP Mazembe kwa sababu tu ya fedha ndogo ya usajili.

Hajawaza mbele, amekomea kuwaza kwenye pesa ya usajili peke yake. Hajawaza maisha ya TP Mazembe ambavyo yanaweza kumnufaisha yeye kama yeye.

Hajawaza namna ambavyo angepata mkataba ambao ndani yake una vipengele vingi vyenye kumwezesha yeye kupata malupulupu kibao.

Hivi hapa Tanzania kuna klabu ambayo ina vipengele ambavyo vinaweza kumwezesha mchezaji apate pesa ya ziada kila anavyofanya kitu cha ziada uwanjani?

Mfano, mchezaji akitoa pasi za mwisho za magoli ?, mchezaji anapofunga Hat trick? Au mchezaji anapokuwa mfungaji bora? Au hata tuseme kipindi timu inapochukua ubingwa wa ligi kuu?

Hapana shaka hakuna klabu inayotoa pesa hizo za ziada kwa wachezaji wetu. Wachezaji wetu hutazama signing fee peke yake na siyo vipengele vilivyo ndani ya mkataba.

Ndiyo maana leo hii Ibrahim Ajib Migomba ameikataa TP Mazembe kwa sababu ya signing fee kubwa aliyoahidiwa na timu ya hapa nyumbani.

Bado anajiona anataka kuendelea kukaa nyumbani, na amekataa kwenda sehemu ambayo inaweza kumwezesha yeye kushinda taji la ligi ya mabingwa barani Afrika, sehemu ambayo inaweza ikampa nafasi kubwa ya kujiuza kuliko hapa nyumbani.

Sambaza....