Sambaza....

Hapana shaka historia kati ya Yanga na Mwinyi Zahera imebaki kwenye maandishi tu. Maandishi yanatuambia kuwa Yanga iliwahi kuwa na Mwinyi Zahera. Kocha ambaye alisimama kama baba wa Yanga.

Baba ambaye alikuwa hapendi kumuona mwanaye akiteseka. Haikujalisha ugumu wa maisha ambayo Mwinyi Zahera aliyakuta ndani ya Yanga, lakini alisimama imara na kuwaonesha yuko tayari kutembea nao kwa nyakati zote.

Miguu yake ilikuwa tayari kukanyaga mawe ya moto akiwa peku , kisa tu viatu vyake alivua na kuwapa Yanga ambao kwa wakati huo walikuwa peku. Alitembea nao kwenye ugumu wote, hakutaka kuwaacha hata kidogo.

Hata kipindi ambacho walilia njaa yeye alikuwa tayari kusimama na kuinua mkono wake kwa ajili ya kuwalisha Yanga. Furaha yake ilikuwa kuwaona Yanga wakitabasanu. Alijitahidi sana kwa hili kuweka tabasamu kwenye nyuso zao.

Na kizuri zaidi kuna kipindi alipewa mahaba mazito na mashabiki wa Yanga, mahaba ambayo yalimfanya apaone Yanga ndiyo Congo halisi , sehemu ambayo kitovu chake kilizikwa. Mahaba haya yalimfanya awe mwepesi kutoa chochote kitu kwa ajili ya Yanga.

Yanga ikaenda kwa kujikongoja lakini dereva yake mkuu alikuwa Mwinyi Zahera. Huyu ndiye alikuwa kocha , mwenyekiti na katibu wa Yanga. Lakini kama ilivyo kwa kila majira kuwa na nyakati zake ndivo ilivyokuwa kwa Mwinyi Zahera.

Majira yake yameisha. Hatuko naye tena Mwinyi Zahera. Tumebaki na Yanga ambayo haiwezi kuondoka. Watu huja Yanga na kuiacha Yanga ilivyo. Mwinyi Zahera kaondoka ila katuachia David Molinga.

Mtu ambaye ana kiwango cha kawaida sana kuchezea Yanga. Yanga inahitaji washambuliaji ambao wanatumia nafasi vizuri ili kuisaidia timu. Hiki kitu hana na amekuwa akifanya makosa ambayo yanaigharimu timu.

Sambaza....