Shirikisho la Soka Afrika CAF lilimteua Ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Cliford Mario Ndimbo kuwa Ofisa habari wa Caf katika mchezo wa klabu bingwa Afrika namba 99 kati ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Asec Mimosas ya Ivory Coast utaopigwa nchini Afrika Kusini Februari Mosi katika uwanja wa Tshwane-Loftus Versfeld.
Akizungumza na KANDANDA, Cliford amesema kuwa kuteuliwa kwake kunadhihirisha kuwa, soka la Tanzania limeanza kupiga hatua.
“Kuteuliwa kwangu kunamaanisha kuwa, CAF wameanza kuiamini Tanzania na watendaji wake, sifa hizi si zangu bali ni za Tanzania nzima nan i kwa ajili ya maendeleo ya soka nchini” alisema Ndimbo.
Si mara ya kwanza kwa Cliford kuteuliwa kuwa Ofisa habari wa CAF katika mashindano mbalimbali, alishawahi kupewa dhamana hiyo zaidi ya mara moja hasa kwa mechi zinazochezwa na hapa nyumbani.
“Nakumbuka mwaka jana kipindi Yanga SC ikishiriki hatua ya makundi, shirikisho Afrika, CAF waliniteua zaidi ya mara moja kuwa Afisa habari wao”
Jukumu kubwa la Ndimbo kama Afisa habari CAF katika mchezo wa Februari Mosi ni kusimamia masuala ya vyombo vya habari na kazi nyingine za kimawasiliano kati ya Shirikisho na wasimamizi wa mechi ikiwemo matokeo, majukumu hayo hayana tofauti kubwa na yale anayoyafanya akiwa TFF.
Akielezea siri ya kupata uteuzi huo, tena zaidi ya mara mbili, Cliford ameseam kuwa, umakini katika kazi ndio unaopelekea kuteuliwa kwake.
“ Unajua uteuzi huu haumaanishi kuwa mimi ni wa kipekee lakini ubora katika kazi ndio sababu, CAF walishawahi kufanmya kazi na mimi zaidi ya mara moja na baada ya mechi lazima uandae ripoti ya kile ulichokisimamia, kwahiyo inaonekana ripoti zangu huwa ziko sawa”.
“hii ni taaluma, hawawezi kukuteua tu eti kisa ni Afisa habari, lazima uonyeshe kuwa upo makini na kazi yako na unajituma” aliongeza Ndimbo.
Imekuwa ni kawaida sasa kwa CAF kuwateua watu kutoka nchini kuliwakilisha shirikisho hilo katika majukumu yake na Cliford Ndimbo ni miongoni mwa watu hao, hii ni dalili njema kwa nchi kuwa imeanza kukubalika kimataifa hasa kwa upande wa rasilimali watu na utendaji kazi wao, ni muhimu kwa wanaopata fursa hizi kutozifanyia makosa. Kila la heri Ndimbo katika majukumu yako.