UKIZITOA timu wenyeji wa michuano Misri, Morocco na Algeria ambao tayari wamekwishacheza na Tunisia wanaotaraji kucheza mchezo wao wa kwanza katika Kundi la Nne, timu nyingine 11 zenye wachezaji ‘weusi’ tu zina tatizo ‘kubwa la kufanana’.
Nje ya tatizo la kimbinu na ufundi, ‘Ball touches’ ya kwanza imekuwa tatizo kubwa kwa timu za Zimbabwe, DR Congo, Uganda, Nigeria, Burundi, Guinnea, Madagascar, Namibia, Senegal, Tanzania, na Kenya na pengine hilo linaweza kuendelea kuonekana katika michezo ya leo – Ivory Coast vs Afrika Kusini , Tunisia vs Angola na Mali vs Mauritania.
HARAMBEE STARS vs TAIFA STARS
Baada ya kupoteza michezo yao ya kwanza ya kundi la Tatu kwa vipigo vya kufanana ( 2-0, 2-0) kutoka kwa Senegal na Algeria, timu hizo za Afrika Mashariki zitakutana zenyewe kwa zenyewe Alhamis ya wiki hii, siku ambayo pia ‘wababe’ wao Senegal na Algeria wakiwa tayari wameshacheza mchezo wao.
Stars na Harambee zilipoteza michezo yao ya jana Jumapili kutokana na sababu kadhaa- kimbinu na kiufundi. Kkenya walionekana wazi ‘waoga wa michuano’ wasio na uzoefu wowote na licha ya kuwa na wachezaji wakali kama straika Michael Olunga, kiungo na nahodha Victor Wanyama, na mlinzi wa kati Musa Mohammed bado walionekana kufanya makossa mengi yaliyopelekea wakacheza faulo nyingi ( 25)
‘Miguso’ yao ya kwanza katika mpira ilikuwa mibaya, na hilo liliwafanya muda mwingi wa kipindi cha kwanza kuutafuta mpira uwanjani. Walibana vizuri goli lao lakini baada ya dakika 30 wakajikuta wakipoteza umakini na wakaruhusu magoli mawili katika robo saa ya mwisho ya kipindi cha kwanza.
Mabadaliko ya haraka mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili yaliyofanywa na kocha, Sebastien Migne dakika ya 46 kwa kumtoa kiungo, Francis Kahata na kumpa nafasi Eric Ouma yaliisaidia mno Kenya na angalau walipandisha kiwango chao cha umiliki wa mchezo kwa asilimia 10+ kutoka 34 hadi 43.
Kitu kizuri nilichokiona kutoka kwa Harambee Stars ni uwezo wa kocha wao wa kuusoma mchezo na mabadiliko ya wachezaji ambao kadri muda ulivyokuwa ukisonga walionyesha kupata uzoefu Zaidi. Mchezo wao wa Juni 27 dhidi ya Stars tunaweza kuona mambo tofauti hasa kiuzoefu baada ya kusumbuliwa mno na ‘Mbwa Mwitu wa Jangwani’ usiku wa jana.
Stars ambao walimaliza mchezo wao dhidi ya Senegal kwa umiliki wa asilimia 39, wanapaswa kubadilika mno hasa kwa benchi la ufundi. Kocha, Emmanuel Amunike alianza sit u na mfumo mbaya, bali hata wachezaji aliwachagua kuanza katika mfumo wa 4-3-3 hawakuwa sahihi.
Mabadiliko yake ya kwanza kufanya ilikuwa ni dakika ya 44 kwa kumtoa kiungo chipukizi Feisal Salum na kumpa nafasi Farid Musa. Haya ndiyo mabadiliko ya haraka Zaidi ya kiufundi kufanywa tangu kuanza kwa michuano hiyo na yalifanywa kwa hofu ya kocha huyo kubaki pungufu uwanjani kufuatia kadi ya mapema ya njano aliyoonyeshwa kiungo huyo wa kati mapema kabisa mwa mchezo.
Stars ilicheza faulo 23 katika mchezo wa jana ( mbili pungufu) ya walizocheza Kenya na nyingi zilifanywa na Feisal. Amunike anapaswa kubadilika haraka kimbinu na kiuchaguzi wa wachezaji -labda sasa anapaswa kumrudisha kikosi cha kwanza Erasto Nyoni, kumpa muda Zaidi Frank Domayo ambaye alionyesha uwezo wake wa kuvusha mipira kwa dakika sita alizompokea Mudathir Yahya.
Namna alivyowapanga nahodha, Mbwana Samatta, John Bocco na Saimo Msuva haikuvutia na wala haikusaidia lolote kwa timu kiujumla. Kama anaona kuna kitu ambacho Bocco anacho kwa dakika 90’ basi Amunike anapaswa kumchezesha katika eneo la mshambulizi wa kwanza na si yule anayetokea pembeni.
Sijui, labda Amunike alihitaji msaada wa Bocco kukaba kuanzia juu upande wa kulia kwa Senegal, ila bado hakutoa msaada uliotakiwa. Kuwapanga Mudathir, Feisal na Himid Mao katika eneo la kati ilikuwa ni kuinyima nguvu Stars katika eneo la kati, lakini bado Amunike anayo nafasi ya kujitazama na kuwatazama baadhi ya wachezaji anaowaacha katika benchi.
Dhidi ya majirani zetu Kenya siku ya Alhamis hii itakuwa bonge la mechi kwa sababu ushindi kwa timu yoyote unaweza kuipeleka timu hiyo katika hatua ya 16 bora na kupoteza itakuwa ni kujiweka Zaidi katika ‘utayari wa kurudi nyumbani’.
Katika ‘washindwa bora ‘ wanne wanaotakiwa kuungana na washindi wa kwanza na wa pili wa makundi ( 12) pointi tatu hadi nne zinaweza kuipeleka timu hatua ya mtoano, lakini je, Amunike yupo tayari kujifanyia mabadiliko ya haraka kama mshindani wake ajaye, Sebastien ?
Harambee vs Stars ni mechi ya ‘Afrika Mashariki’ na si mechi ya marudio ya zile nyingi ambazo wameshakutana, ni ‘vita’ , vita hasa ya kwenda kutengeneza rekodi mpya kwa kila timu kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza. Haijalishi kwa njia ya ‘tundu la sindano’ ama ushindi wa kundi.