Sambaza....

Wako wapi, Abuu Ubwa na Haruna Chanongo? Kwanini Said Ndemla bado anaendelea kuchezea Simba SC wakati iliripotiwa alifuzu majaribio yake huko Sweden mwanzoni mwa mwaka huu? Nini kinaendelea kumfanya Thomas Ulimwengu aendelee ‘kutangatanga’ kimpira tangu alipolazimisha kuondoka TP Mazembe Septemba 2016?

Maswali yote haya najiuliza na ninayo majibu ya msingi, lakini ningependa kumshauri kiungo mshambulizi wa Simba SC, Adam Salamba naye ajiulize maswali hayo wakati huu meneja wake Jamal Kisongo ‘akicheza’ na baadhi ya vyombo vya habari kuwaaminisha watu kwamba Salamba anafuatiliwa na yupo katika mipango ya kwenda Anderletch ya Ubelgiji.

CHANONGO NA UBWA


Miezi 26 iliyopita Chanongo na Ubwa walikwenda kufanya majaribio TP ya DR Congo na baadae meneja wao Kisongo akasema wachezaji hao walifanya vizuri katika majaribio yao na wangesainiwa Mazembe. Wakati huo, Chanongo alikuwa mchezaji wa Mtibwa Sugar FC ( ambako bado yupo hadi sasa) na Ubwa alikuwa Stand United ya Shinyanga.

Unajua uongo una kawaida ya kuwahi sana kuliko ukweli wenye tabia ya kuchelewa na nakumbuka wakati wachezaji hao wameenda TP na kurejea nchini, Kisongo alidai wamefanikiwa na wataichezea klabu bingwa hiyo mara tano kihistoria Afrika. Hakuna kilichoendelea.

Hivi sasa Ubwa yupo Reha FC timu ya daraja la kwanza Tanzania Bara na Chanongo anaonekana yupo mbali na sifa za mchezaji wa kulipwa tangu alipoondolewa Simba miiaka minne iliyopita kwa sababu ambazo awali zilidai ni kumfanya awe huru ili kurahisisha mipango yake ya kwenda kucheza nje ya nchi.

Kwa mtazamo wangu wa Mbali, wachezaji hawa wawili wenye vipaji wanashindwa kufikia malengo yao ya kimpira licha ya vipaji vikubwa walivyopnavyo kutokana na usimamizi mbovu wa meneja wao. Kisongo anapaswa kubadilika kama kweli ana nia ya dhati ya kuendeleza vipaji vya wachezaji anaowasimamia.

Kama inatokea nafasi ya wachezaji wake kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ni vyema lakini kuzungumza sana na vyombo vya habari kabla ya mambo kuwa sawa ni jambo linalowapotezea malengo wachezaji husika. Hawezi kukwepa lawama kuhusu TOM na na alishindwa kuwa mkweli baada ya Ndemla kutoka Sweden Januari mwaka huu.

NDEMLA


Mfano, Ndemla alipompeleka Sweden alisema ndiyo kipindi cha usajili lakini kiukweli wakati mchezaji huyo anatua katika nchi hiyo ya Scandinavia ligi za huko zilikuwa zimeashaanza na hakukuwa na nafasi yoyote ya kusainiwa wachezaji wapya. Ndemla aliporejea alijikuta akipoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha Simba na hadi sasa mchezaji huyo anaendelea ‘kudumaa’ kimpira.

Ndemla

SALAMBA


Atulize akili yake na kufanya kazi kwa bidii klabuni Simba. Kama ataingia katika mawazo ya kwenda Anderletch namuakikishia atapoteza kila kitu. Hana uwezo wa kucheza Ubelgiji kwa sasa tena kwenye klabu kubwa zaidi nchini humo. Unaweza vipi kusajiliwa Anderletch wakati hata katika soka la ndani ameshindwa kucheza katika klabu yake?

Kisongo atampoteza mchezaji huyu mwenye kipaji kama alivyofanya kwa Tom ikiwa mchezaji mwenye atahamisha mawazo yake kutoka Simba na kwenda huko anakofikirishwa. Salamba atakuwa mchezaji muhimu kwa Simba kama ataendelea kujituma katika klabu hiyo, amini hiki nisemacho, lakini akijaribu kuwaza ulaya kabla ya kujikuza kimpira bongo bila shaka misimu miwili au mitatu zaidi atakuwa timu ya chini kama ilivyo kwa Ubwa.

Kukaa kimya na kufanya mipango ya kimya kimya inaweza kuwa faida kubwa kwa Kisongo, anaweza kuendelea kuwatafutia dili wachezaji wake lakini anapaswa kujiuliza pia kwanini wengi wanaporomoka wakiwa chini yake tena wangaii vijana wadogo?

Sambaza....