Klabu ya Arsenal imepigwa faini ya zaidi ya Shilingi Milioni 61 na chama cha soka England (FA) kwa kosa la wachezaji wake kumzonga Refa Graham Scott kupinga pigo la penati katika mchezo wa ligi ya England dhidi ya Leicester City mapema mwezi huu.
Wachezaji wa Arsenal walimzonga refa Scott kupinga faulo iliyochezwa na Henrikh Mkhitaryan kwa mchezaji Demarai Gray katika dakika ya 75 wakati ambapo mchezo ukiwa sare ya bao 1-1 ambapo penati hiyo ikafungwa na Jamie Vardy kuwapa uongozi Leicester City kabla ya Riyad Mahrez kufunga la ushindi baadae.
Taarifa ya FA imesema wametoa hukumu hiyo baada ya klabu kushindwa kuwazuia wachezaji kuonesha adabu katika mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa King Power.
“Arsenal wamekubali kuwa walitenda kosa lakini wamekataa idadi ya faini waliyotozwa, Tume huru ya udhibiti ilifanya kazi yake na hatimaye ikakubaliana kutozwa kwa faini hiyo, kwa kosa walilolifanya” Taarifa ya FA imeeleza.