TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Jumapili hii inataraji kucheza mchezo wake wa kwanza wa fainali za kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kupita Zaidi miaka 39 kwa kuwavaa washindi wa pili wa michuano hiyo miaka ya katika 1992 na 2002, Senegal katika mchezo wa kundi la Tatu huko nchini Misri.
Kuelekea mchezo huo utakaopigwa saa mbili usiku kwa saa za Tanzania, Stars imecheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya wenyeji wa michuano hii Misri na timu nyingine ya Kusini mwa Afrika- Zimbabwe. Je, ni majaribio ambayo yanaifanya Stars kuwa tayari kwa michuano hiyo mikubwa?
Katika michezo hiyo miwili ambayo kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike alitumia Zaidi ya wachezaji 22 tofauti na hii inampa fursa msindi huyo kiuchezaji wa michuano hiyo mwaka 1994 akiichezea Nigeria nafasi ya kutambua kwa ukaribu wachezaji alionao kikosi na vile wanavyoweza kumpa matokeo.
Amunike amepata pigo la kwanza katika mbinu zake wakati wa mchezo dhidi ya ‘Pharaohs’ kwa kumpoteza mlinzi wa kati na mfungaji wa moja ya magoli matatu ya Stars katika mchezo wa mwisho wa kuwania kufuzu dhidi ya Uganda, Machi mwaka huu-mlinzi wa kati, Aggrey Moris ambaye aliumia katika game hiyo Stars waliyochapwa 1-0.
Tayari Amunike amemuita kikosi mlinzi David Mwantika kama mbadala wa Aggrey na kuungana na walinzi waliokuwepo kikosini Kelvin Yondan na Ally Mtoni ‘Sonso’ kama walinzi katika beki ya kati. Katika kundi ambalo pia Stars itakutana na Algeria na majirani zetu Kenya ambao usiku wa Jumapili pia watakuwa uwanjani katika mchezo mwingine wa kundi C.
SOKA LA KUJILINDA…….
Katika michezo mitatu , timu inayoweza kupata alama tatu pia inaweza kufuzu kwa hatua ya 16 bora kutokana na kwamba kutakuwa na nafasi nne za ‘washindwa bora’ ambao wataungana na timu 12 zitakazomaliza katika nafasi mbili za juu ili kutengeneza idadi ya timu 16 katika hatua ya kwanza ya mtoano.
Soka la kujilinda linaloambatana na mbinu ‘Ant-Football’ ndilo linaweza kuisaidia Stars katika michuano hii. Kitu muhimu hata kama watapoteza mchezo hawapaswi kuruhusu magoli mengi. Wakati ‘Mbwa Mwitu wa Jangwani’ wakicheza na ‘Harambee Stars’ Jumapili hii, mechi ya Stars dhidi ya Kkenya inaweza kutoa ‘mshindwa bora’ katika kundi la tat una hapa kwa timu itakayozuia vizuri dhidi ya Senegal na Algeria ndiyo itakuwa na nafasi ya kupita kwa kutumia ‘tundu la sindano’.
MASHAMBULIZI YA KUSHTUKIZA
Amunike anao wachezaji ambao kama wakielekezwa vizuri jinsi ya kujilinda anaweza kusonga mbele lakini huwezi kupata matokeo kama hutafunga goli/magoli ya kutosha. Stars ilifunga goli kupitia nahodha Mbwana Samatta katika mchezo was are ya 1-1 dhidi ya ‘Warriors’.
Wakati Kenya ikifunga magoli katika kila mchezo waliojipima nguvu dhidi ya Madagascar 0-1 Kenya, DR Congo 1-1 Kenya, huku Algeria wakifunga magoli manne katika game mbili za kujipima, Algeria 1-1 Burundi, Algeria 3-2 Mali na Senegal wakifunga mara tatu katika game mbili dhidi ya Senegal 2-1 Mali, Senegal 1-0 Nigeria ni lazima Stars iongeze ufanisi katika namna ya kushambulia.
Kuwatumia, Saimon Msuva, Mbwana Samatta kama washambuliaji pekee itasaidia sana Stars katika mashambulizi ya kushtukiza ‘counter attack’ kutokana na kasi ya wachezaji hao . kuwatumia wawili hawa kama washambuliaji pekee kutatoa nafasi ya Amunike kuwachezesha Mwantika, Sonso na Kelvin kwa pamoja katika eneo la beki ya kati.
Hassan Kessy katika beki ya kulia, Gadiel Mmichael katika beki tat una walinzi hao watatu wa kati wanaweza kutengeneza ngome ya watu watano ambayo ni sahihi mno kwa Stars. Kuwapanga Himid Mao, Farid Mussa, na Mudathir Yahya katika kiungo na Samatta na Msuva katika eneo la mbele kutaifanya timu hiyo kuwa ngumu kufungika huku pia ikiwa na uwezo wa kupata goli/magoli kutokana na mashambulizi ya kushtukiza watakayokuwa wakiyaandaa.