Moja ya wachambuzi wakubwa wa soka hapa nchini Tanzania amenukuliwa juu ya ukweli wa kitu kinachoisibu Azam FC na kushindwa kuwa timu inayoweza kubeba ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara ( NBC Premie League ), Jemedari alisema maneno yafuatayo.
“Azam hii wakati inashinda mechi kadhaa ikiwa chini ya Abdul Moalin tulisifu, wakati inanyimwa penati katika mechi dhidi ya Mbeya City pia tulisema, ilifungwa bao na kipa akasema kuwa si bao tulisema kuwa ni bao, Azam sio kubwa na haina huo ukubwa uwanjani, Azam ingekuwa kubwa mijadala isingeepukika, leo tunaijadili Geita kwa sababu wana mfungaji, je Azam ina nini timu ambayo imekuwa nyepesi na kufungwa na Polisi nyumbani na ugenini?, habari za kulalamikia penati na waamuzi zinawahusu bodi ya ligi sisi hazituhusu, lakini swali ni je mliwahi kulalamika?”.
Twende hapa sasa, tayari ligi kuu ya NBC imeshapata bingwa wa msimu huu wa 2022-2022 na kilichobakia ni kuzifahamu timu zitakazoshuka daraja na kucheza ligi ya Championship msimu ujao, Azam ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri lakini kwa bahati mbaya panda shuka ya viwango imekuwa ikitawala katika mitaa hiyo ya Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Kwa jinsi mazingira yalivyo mpaka sasa ni vyema Azam wangekuwa na malengo mawili makubwa, lengo la kwanza ni kuhakikisha wanamaliza katika nafasi nzuri ili kupata tiketi ya uwakilishi wa nchi katika michuano ya kimataifa ya CAF na lengo la pili wautazame sana msimu ujao ni namna gani wataisuka timu yao ili iwe yenye ushindani na kuchukua taji la ubingwa, inaweza kuwa ni vigumu lakini si kama haiwezekani.
Twende kwenye mada ya msingi, tukiatazame Azam ni kwanini imekuwa timu inayokosa muendelezo wa matokeo mazuri, anguko la kwanza kwao ni katika machaguo ( scouting ) ya wachezaji wa kigeni, ukiwatazama Azam wachezaji wao wa kigeni wengi wanashindwa kucheza katika daraja ambalo linaweza kuwatofautisha na wachezaji wazawa.
Ukiwatazama wachezaji wetu wazawa wengi wao hawana utofauti mkubwa wa ubora, hata ukiangalia ubora wa wachezaji waliopo katika timu hizihizi kubwa za Simba na Yanga ni ubora huohuo unaopatikana Kagera Sugar, KMC, Coastal Union na klabu nyingine za daraja kama hilo, itoshe kusema wachezaji wengi wazawa wanafanana ubora wao.
Tujiulize swali dogo, ni wapi utampata Yannick Bangala katika ardhi hii ya Tanzania? wapi utampata Meddie Kagere ambae atakuwa goli 40 ndani ya misimu miwili? wapi utampata Djuma Shabani? lakini tukisimama kwenye uhalisia ni rahisi kumpata mbadala wa Dickson Ambundo, Yassin Mustapha, Zawadk Mauya, Kibu Dennis katika ardhi hiihii ya Tanzania tofauti na ubora mkubwa unaotoka nje.
Anguko kubwa la Yanga katika misimu minne lilitokana na kukosa wachezaji bora kutoka nje, hiyo ndio sababu namba moja, anguko la Simba msimu huu limetokana na tatizo hilohilo pia baada ya kukosa watu sahihi wa kuziba nafasi na wageni wengi waliobaki ndani ya timu wameshindwa kuleta utofauti.
Azam wanapaswa kufanya chaguzi nzuri ya wachezaji wa kigeni ambao wataleta kitu tofauti na kile ambacho wazawa wanatoa, leo Yanga wanatamba kwa sababu walifanya chaguzi nzuri ya wachezaji wa kigeni ambao wameleta utofauti, leo Simba wanateseka kwa sababu walifanya chaguzi ya wachezaji wengi wa kigeni ambao hawajaleta utofauti, ukiacha wachezaji wachache wenye vitu vya ziada wachezaji wetu wengi wazawa wanafanana ubora na ni rahisi kupata wanadala wao ndani ya nchi, lakini wapo wachezaji kutoka nje ambao ukiwaingiza ndani ya timu inakuwa chachu kwa wachezaji wazawa kuboresha viwango vyao.
Kipo kichaka cha kijifichia kwa Azam ya kuwa wanaonewa kutokana na maamuzi mabovu ya marefa, inawezekana kukawa na ukweli lakini hili si tatizo namba moja ambalo linawafanya Azam wafanye vibaya kwenye ligi, tatizo la msingi ni wao wenyewe, kila timu inaonewa kwenye ligi, si Yanga ambae ni bingwa wala si Simba anaeshika nafasi ya pili hivi sasa, makosa hutokea kwa kila mmoja anaeshiriki ligi kuu.
Ni vyema kama viongozi wa Azam wataachana na fikra za wao kuonewa na watengeneze timu, ukiwa na timu unaweza kuangushwa na maamuzi mechi ya leo na ukashinda mfululizo katika mechi zijazo, hivi ndivyo timu yenye sifa ya ubingwa hufanya.