Sambaza....

Yondani amedumu katika kiti cha unahodha kwa miezi 6 pekee kabla ya kitambaa hicho kupewa Ibrahim Ajib Migomba.


Baada ya aliyekuwa nahodha wa Yanga Nadir Haroub Canavaro kustaafu soka, mwezi July mwaka 2018 na kupewa jukumu la Umeneja, kitambaa chake kilichukuliwa na Kelvin Yondani.
Yondani alipewa wasaidizi wawili ambao ni Juma Abdul Mnyamani na Thaban Sikala Kamusoko ambao wangemsadia katika majukumu yake ya Unahodha.


Lakini matukio ya nidhamu mbovu ya Kelvin Yondani yalimfanya Zahera kumvua kitambaa hicho na kisha kumvisha Mr. Assist, Ibrahim Ajib hii ilikuwa ni mwezi wa kwanza mwaka 2019 kabla ya mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga.

Kwa sasa, klabu ya Yanga haina nahodha. Kuna watu wanatamani nafasi ya unahodha ingekuwa anapewa mtu yeyeto hata kama sio mchezaji lakini tafsiri halisi ya nahodha ni kiongozi wa wachezaji ndani na hata nje ya uwanja.
Cheo cha unahodha hupewa mchezaji anayeheshimika na wachezaji wengine wote na anayeaminika kuwa anaweza kuwaongoza wengine kufanya vizuri kwa faida ya klabu.

Nahodha anategemewa kuwa muhimili mkubwa kwa timu wakati wa kipindi kigumu timu inapopitia, yaani yeye ndio atakuwa kiigizo za kushusha presha kwa wachezaji wenzake.
Hivi karibuni mchezaji wa Manchester United na timu ya taifa ya Hispania, Davis De Gea ameamua kujipigia upatu mwenyewe juu ya kuutaka unahodha wa klabu yake. Katika hoja zake za msingi alizoziona kwanini anastahili kuwa nahodha ni muda alioitumikia klabu hiyo.

De Gea amekuwa na Man U tangu mwaka 2011, na mwenyewe anahisi hata damu yake sasa ina mapenzi ya dhati na klabu hiyo na yupo tayari kuipigania.
Kwa maana hiyo hata nahodha wa Yanga, sharti kwanza awe anaijua yanga na ameitumikia kwa kipindi Fulani, kuijua yanga kwa upande wa falsafa, miiko ya klabu, tamaduni zake na mengine yote yuanayoihusu klabu.

Kwa upande wangu nitawaangazia wachezaji watano wa Yanga ambao ni Kelvin Yondani, Juma Abdul Mnyamani, Mrisho Ngasa Anko, Deus Kaseke na Papy Tshishimbi.

Wachezaji hao wote wameitumikia Yanga zaidi ya misimu miwili, nitakupa sifa 4 za mchezaji kuwa nahodha na sifa hizo nitazitumia kuwachambua wachezaji hawa watano hadi tupate mmoja.

Kitu muhimu cha tahadhali juu ya hili ni lazima tukumbuke kuwa unahodha haupigi kura, yaani ni kocha anakuteua tu. Kama ni jukumu la kocha kumteua nahodha maana yake mchezaji lazima amshawishi kocha katika mazingira yote wanayokutana yaani kipindi cha mazoezi, mechi, na maisha nje ya uwanja.


1.Nidhamu ya nje na ndani ya uwanja.

Neno nidhamu ni neno pan asana, lina vitu vingi sana lakini naweza sema mchezaji lazima awe na heshima kwa viongozi na wachezaji,kujiheshimu ili aheshimiwe na wengine, kujiamini na kuamini kipaji chake.
Mchezaji lazima aheshimu mazoezi, auheshimu mwili wake kwa kuupa chakula bora kitakachomfanya afanye vizuri, lazima ajali maendeleo ya kazi yake kikwelikweli, yaani ajitume.


Katika hili naweza kuwakadilia hivi

Kelvin Yondani-45%
Juma Abdul Mnyamani – 55%
Mrisho Ngasa Anko- 80%
Deus Kaseke- 74%
Papy Kabamba Tshishimbi-85%


2. Mawasiliano

Ukitaka kuwa nahodha pia lazima uwe muongeaji. Yaani uwe na uwezo wa kuelekeza wenzako kwa kupiga kelele uwanjani, kuwakumbusha majukumu yao, pia kuwa mwepesi kuwatetea, hasa katika matukio yanayohusisha maamuzi ya kadi kutoka kwa refa.
Wengi wanaamini aina ya wachezaji wanaocheza nafasi ya beki wa kati huwa na uwezo mkubwa wa kuongea na wachezaji kwa sababu jinsi wanavyouona uwanja na wachezji wote, mfano wa manahodha wakubwa katika nafasi hiyo ni Sergio Ramos, Thiago Silva, Puyol, Gary Cahill, John terry, Nemanja Vidic.


Kama ulishawahi hudhuria mazoezi ya Yanga, na ukamuona mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Thabani Sikala Kamusoko utaelewa hii hoja ya kuwa muongeaji wakati wa mazoezi.
Kamusoko alikuwa anapiga kelele zile za, pigaa, unakuibaa.. Nipo nyumaa…. Enheee, turnnniii…


Katika hoja nawapa hivi..
Kelvin Yondani-95%
Juma Abdul Mnyamani – 40%
Mrisho Ngasa Anko- 49%
Deus Kaseke- 42%
Papy Kabamba Tshishimbi-20%


3. Kuwa na sifa za kiuongozi.

Hapa mchezaji ni lazima amshawishi kocha kuwa yeye anastahili kuwa kiongozi kwa wengine. Kocha atakujua tu kama una dalili za kuwa kiongozi au la.
usitatue vitu kimihemko, kuwa mfano kwa wengine, mchezaji lazima awe na uwezo wa kutia moyo wachezaji hasa katika kipindi kigumu. Kipindi ambacho timu iko nyuma kwa goli 2 na inahitaji kurudi mchezoni, kipindi ambacho klabu imeyumba kiuchumi, kila mchezaji anadai chake. Kiongozi lazima ajiamini.
Yaani ajiamini yeye, uongozi wake, kocha wake na wachezaji wenzake, lazima awaanini kuwa wanaweza kuleta ushindi muda wowote bila kujali hali iliyopo ndani ya timu au klabu.

Katika hili.


Kelvin Yondani-70%
Juma Abdul Mnyamani – 55%
Mrisho Ngasa Anko- 50%
Deus Kaseke- 44%
Papy Kabamba Tshishimbi-40%

4. Muendelezo.

Mchezaji anayestahili kuwa nahodha lazima awe na muendelezo katika mambo yote tuliyataja hapo juu. Lazima apambane na vikwazo vyote kuhakikisha anazifikia hoja za hapo juu.
Yaani kama ni nidhamu lazima iwe na muendelezo, kama busara na kujituma lazima pia kuwe na muendelezo, sio leo mchezaji anakuwa na sifa Fulani baadae anabadilika.


Katika hili..
Kelvin Yondani-70%
Juma Abdul Mnyamani – 75%
Mrisho Ngasa Anko- 80%
Deus Kaseke- 77%
Papy Kabamba Tshishimbi-80%


Kwa mujibu wa makadilio yangu, mwisho kabisa wachezaji hawa watakuwa wamepata hivi;


  1. Kelvin Yondani- 270%= 67.5%
  2. Mrisho Ngasa Anko- 259%= 64.8%
  3. Deus Kaseke- 237%= 59.3%
  4. Juma Abdul Mnyamani – 225%= 56.3
  5. Papy Kabamba Tshishimbi-220%= 55%

Kwa matokeo haya, Yanga isione aibu kurudisha kitambaa kwa waliompokonya mwanzo. Huwezi ukamkuta mchezaji aliyetimia kuwa nahodha kwa timu yenye mikwamo mingi ya kifedha kama Yanga.

Binafsi naamini kuwa, kati ya Kelvin Yondani, Mrisho Ngasa na Deusi Kaseke mmoja wao anaweza kuwa nahodha wa Yanga.

Sambaza....