Sambaza....

Kocha mkuu wa kikosi cha timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Emmanuel Amunike amesema wataangalia makosa ambayo waliyafanya hadi kufungwa mabao 3-0 na Cape Verde na kuyarekebisha kabla ya mchezo wa Jumanne.

Amunike amesema licha ya kufungwa lakini bado wanamchezo mwingine siku ya Jumanne na wanatakiwa kuangalia makosa yaliyojitokeza na kuyarekebisha kabla ya mchezo huo utakaofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

“Bado tunamchezo Tanzania, tutaangalia makosa yetu na kuangalia namna ya kuweza kuyasahihisha kabla ya Jumanne, kundi hili bado lipo wazi, Cape Verde wana alama nne, sisi tunazo mbili kama tutashinda siku ya Jumanne tunaweza kuwa na alama tano,” amesema.

Amunike amesema walijipanga vizuri kushinda mchezo huo lakini wamepoteza na kinachopaswa kwa sasa ni kuhakikisha wanapunguza makosa yaliyojitokeza kwani bado Cape Verde ni wazuri.

“Kipindi cha pili wachezaji walicheza vizuri kidogo lakini kipindi cha kwanza katika dakika za mwanzoni tulishindwa kucheza vizuri, tulipoteza umakini na kuruhusu kufungwa magoli marahisi sana,” amesema.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa Mali, Boubou Traore, Drissa Kamory Niare na Baba Yomboliba, mabao yaliyoizamisha Taifa Stars yamefungwa na mshambuliaji wa klabu ya Partizan ya Ligi Kuu ya Serbia, Ricardo Jorge Pires Gomes na beki wa MOL Vidi FC ya Hungary Ianique dos Santos Tavares maarufu kama Stopira.

Cape Verde inapanda kileleni kwa wastani mzuri wa mabao baada ya kufikisha pointi nne, sawa na Uganda ambao leo watacheza mechi ya tatu na Lesotho yenye pointi mbili sawa na Tanzania.

Sambaza....