Penzi zito ambalo wachezaji wa timu ya Taifa wanalipata kutoka kwa mashabiki ndilo lililokuwa linanishangaza wakati niko uwanjani nikitazama mechi ya Taifa Stars na Sudan. Sikio langu lilikuwa makini sana kusikiliza kila neno la upendo lililokuwa linatoka kwenye vinywa vya mashabiki wa Taifa Stars kwa wakati huo.
Wakati wa kutangaza vikosi ndiyo wakati ambao niliamini mashabiki wana mapenzi na timu ya Taifa na siyo mapenzi ya mchezaji mmoja mmoja. Kila jina lililokuwa linatajwa shangwe ilikuwa inaibuka jukwaani. Haya ni mahaba mazito na yanayojitosheleza, mahaba ambayo yanaonesha Watanzania wanaipenda timu yao sana.
Timu ambayo haijawahi kutoa furaha ya kudumu kwa mashabiki. Furaha huja kwa vipindi kama vipindi vya mvua. Mashabiki hawajawahi kupata furaha ya muda mrefu.
Wana mapenzi mazito sana. Mapenzi ambayo yalitakiwa kulipwa na matokeo bora. Tumekuwa tukihangaika sana kupata sehemu ambayo inaweza kutupa furaha lakini mwisho wa siku hakuna tunachokipata.
Tulimuita Emmanuel Amunike, akaja tukamwamini kupita kiasi na akaweza kutupa zawadi ya kwenda kushiriki Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39.
Kipindi cha Emmanuel Amunike timu ilikuwa inacheza soka lisilovutia. Soka ambalo lilikuwa linaumiza kichwa hata kulitazama kwa wakati huo. Ndicho kipindi ambacho timu ilikuwa inacheza soka la kujilinda zaidi lakini ilikuwa inafanikiwa kufunga angalau magoli mawili kwenda mbele. Tuliweza kuifunga Cape Verde hapa goli 2-0, tukaifunga Uganda goli 3-0, tulienda Afcon na kufunga magoli mawili ndani ya mechi tatu ngumu.
Hali ni tofauti kwa sasa. Tangu Ettiene Ndaragije apewe timu, amaefanikiwa kufunga magoli mawili pekee kwenye mechi tano. Magoli ambayo tuliyapata kipindi cha Emmanuel Amunike wakati tuko Afcon.
Pamoja na kwamba kwa sasa timu inacheza mchezo wa kuvutia kuliko kipindi cha Emmanuel Amunike lakini haina uwezo wa kufunga kama ambavyo ilikuwa inacheza chini ya Emmanul Amunike .
Kwanini? , Emmanuel Amunike mara nyingi alikuwa anaamini kushambulia kupitia pembeni ndiyo maana alikuwa anatumia wingbacks. Na magoli mengi ambayo tulikuwa tunayapata yalikuwa yanatoka pembeni.
Wakati huo katikati ya uwanja tulikuwa tunajaza viungo wengi wenye asili ya kuzuia. Hapana shaka pamoja na kwamba tunauhaba wa wafungaji kwenye nchi yetu lakini pia tuna uhaba wa viungo wanaotengeneza nafasi za kufunga.
Ndiyo maana utengenezaji wa mashambulizi ya Taifa Stars kipindi cha Emmanuel Amunike walikuwa wanatengeneza kupitia pembeni kwa wakati huo.
Hii ni tofauti sana na kipindi hiki ambacho tunajaza viungo wengi ambao kwa asilimia kubwa hawana sanaa nzuri ya kutengeneza magoli kwa washambuliaji.
Nafasi ambazo zimetengenezwa kwa sasa ni nafasi ambazo huwezi ukasema ni nafasi wazi za magoli. Ndiyo maana inakuwa ngumu kwa sisi kufunga magoli mengi.
Mwisho wa siku tunajikuta tunaburudisha jukwaa na kuacha kuburudisha nyavu ambazo ndizo huamua furaha ya Watanzania wengi wanaoipenda timu yao.