Sambaza....

June 3 2023 ndio siku ambayo Zlatan Ibrahimovic alituma ujumbe mzito kwenda kwa wapenzi wa Kandanda kote duniani akikanyaga nyasi za San Siro za klabu yake pendwa zaidi duniani AC Milan

Zlatan ameuambia umma wa Kandanda kwamba anaachana na kucheza soka na sasa anatundika daruga zake rasmi akiwa na umri wa miaka 41, ndio mbabe na mjivuni huyu wa Sweden amestaafu rasmi kucheza soka.

Si taarifa yakushtua ama kushangaza kutokana na umri wake, maana lilikua ni jambo la kutarajia kutokana na umri wake lakini pia majeruhi yalimkamata hivi karibuni akiitumikia Milan.

Zlatan Ibrahimovic akiagana na mashabiki wa AC Milan katika Dimba la San Siro.

Binafsi kwangu mimi huyu ndie mchezaji wangu bora wa kandanda duniani, ndio kwangu mimi Zlatan ni bora mbele ya Ronaldo, Messi, Haaland na wengine wengi, usishangae kila mtu na akipendacho.

Zlatan utake nini usipate kutoka kwake katika uwanja ndani ya dakika 90!? Magoli maridadi kabisa, control ya mpira, skills zakutosha, ubabe na zaidi ya yote nje ya soka huyu bwana ni mjivuni na mjeuri haswa. Ni vitu ambavyo binafsi vinanivutia kutoka kwake.

Wanasema ukijua mpira lazima uwe jeuri kidogo wale wachezaji wa “basic football” wasio na vipaji vikubwa ni lazima uwe mnyenyekevu na mwenye nidhamu kubwa na haya ndio maneno ya kijiweni ambayo Zlatan ameyathibitisha. 

Zlatan Ibrahimovic akifunga katika mchezo dhidi ya England. Ni miongoni mwa aina ya ufungaji wake akiwa katika ubora wake.

Dunia ikiwa inazidi kukumbwa na uhaba wa washambuliaji asili leo mshambuliaji mwingine asili kabisa akiwa na sifa zote za ushambuliaji anaachana na kucheza soka, nawewe unajiuliza kama ambavyo mimi najiuliza, Yuko wapi Zlatan mwingine?, Nani atakuja kuvaa viatu vya Zlatan? Jibu ni hakuna, mimi binafsi sioni anakaribia wala kumsogelea huyu bwana walau hata nusu.

Dunia imemshuhudia Karim Benzema, Robert Lewandowsky, Harry Kane, Diego Costa, Lautaro Martinez na hawa kina Kylian Mbappe, Victor Osimhen na Erling Haaland lakini bado huioni kariba ya Zlatan miongoni mwao.

Si tu anafunga bali anafunga mabao mazuri, anajua kuuchezea mpira, anajua kuburudisha na ni ile aina ya washambuliaji wababe ambao mabeki huwa wanawahofia kukutana nae. 

Zlatan Ibrahimovic akiruka na kumdhibiti kwa kisukusuku “kipepsi” mlinzi Tyrone Mings wa Bournemuoth.

Mwamba akiwa na rekodi mbalimbali za mabao lakini hii moja ndio iliyonivutia zaidi, Zlatan ndie mchezaji aliefunga bao katika kila dakika ya mchezo wa soka akiwa uwanjani (anashare rekodi hii na Ronaldo). Kwa maana kwamba katika uchezaji wake soka amefunga goli katika kila dakika kuanzia dakika ya kwanza mpaka ile ya 90.

Akiwa mfungani bora wa muda wote wa Taifa lake la Sweden (mabao 62), mfungaji bora namba tatu wa muda wote wa PSG akifunga mabao 156 katika michezo 180, mfungaji bora namba 5 wa LA Galaxy akiifungia mabao 53 na pia akiwa ndie mfungaji bora wa AC Milan katika Seria A naabao yake 73. Utaona ni mshambuliaji wa aina gani.

Kote alipopita Malmo, Ajax Amsterdam, Juventus, Inter Milan, Manchester United, LA Galaxy, PSG na AC Milan ameacha alama kubwa na historia kubwa katika klabu.

Zlatan Ibrahimovic akiagwa na wachezaji wenzake wa AC Milan.

“The time has  come to say goodbye to football” akisema Zlatan akimaanisha  “Wakati umefika wa kusema kwaheri kwa soka”. Wanakandanda watakukumbuka, dunia itakukumbuka. Zlatan Ibrahimovic ni mmoja tu! 

Tuendelee kusubiri baada ya baada ya kuondoka Zlatan ametuachia nani!?

 

Sambaza....