Sambaza....

Beki wa Timu ya soka ya Stand United ya mkoani Shinyanga Ally Ally amesema ataendelea kuitumikia timu yake katika msimu ujao wa ligi licha ya Vilabu kadhaa kuonesha nia ya kuhitaji huduma yake.

Ally ambaye alijiunga na Stand United akitokea timu ya soka ya Gulioni ya Zanzibar amesema kama itakuwa na ulazimu wa kuondoka Stand basi hatojiunga na timu kubwa kwa msimu ujao kwani bado anahitaji muda mwingi wa kucheza na anaamini akienda timu kubwa hatopata nafasi hiyo.

“Kwa kifupi sitarajii kuondoka Stand, kwa sababu unajua mimi bado mtoto, halafu nikienda hizi timu kubwa naweza kupoteza muda, ukiangalia wanavyofanya usajili unaweza kwenda na wakakudharau ukakosa nafasi ya kucheza,” Ally amesema.

Aidha Ally amethibitisha kutafutwa na viongozi timu mbili mpaka sasa kuomba saini yake ikiwemo Kinondoni Municipal Council pamoja na Mbao FC ya Mwanza lakini amesema bado hajaamua kuondoka Stand kwani anamkataba nao.

“Timu mbili tayari, timu moja hii iliyopanda KMC na Mbao, hao wamenipigia simu na nimeongea nao na nikawaambia bado wasubiri nifuatilie mambo kadhaa, lakini mimi bado ninamkataba na Stand United,” Ally ameeleza.

Kuhusu kutakiwa na Azam FC ya jijini Dar es Salaam, Ally amesema mpaka sasa hiyo imebaki kuwa ni tetesi tu kwani bado hajatafutwa na viongozi wa klabu hiyo, na kama atatafutwa atakuwa na jibu moja tu la kuwaomba wamsubiri amalize mkataba wake na Stand United kwa maana ya kuwepo klabuni hapo msimu ujao.

Ally mwenye umri wa miaka 19 amekuwa ni kivutio kikubwa kwa wapenzi wa kandanda nchini hali iliyopelekea kutabiriwa na wengi kuondoka klabu hapo na kujiunga na timu kubwa, vikiwemo vilabu vya Kariakoo kwa maana ya Simba na Azam, huku Singida United na Azam navyo vikihusishwa na beki huyo.

Sambaza....