Sambaza....

Klabu ya soka ya Alliance ya jijini Mwanza chini ya kocha Malale Hamsini Keya imeendelea kujifua katika uwanja wa Nyamagana uliopo katikati ya jijini la Mwanza kwa ajili ya michezo ijayo ya ligi kuu soka Tanzania Bara.

Malale ambaye hajashinda mchezo wowote toka alipochukua kijiti cha kocha Mbwana Makata aliyetimuliwa kutokana na matokeo mabovu, amekuwa akifanya mazoezi ya nguvu na kikosi hicho ambacho matajario yake ni kuona anapata matokeo chanya katika mchezo wa Jumapili dhidi ya Biashara United.

Afisa Habari wa Alliance Jackson Luka Mwafulango amesema kama klabu wanaendelea kuamini kile ambacho kinafanywa na kocha Malale kitawasaidia kuibuka na ushindi katika mchezo huo wa nyumbani.

“Tunaendelea na maandalizi kuelekea mchezo wa Jumapili dhidi ya Biashara United, tunajua mchezo utakuwa mgumu kutokana na nafasi ambazo kila timu ipo, timu imeendelea na mazoezi na kubwa zaidi tunaendelea kuamini kuwa kocha Malale atatuvusha hapa tulipo kwa kupata matokeo kwenye uwanja wetu wa nyumbani,” amesema.

Katika hatua nyingine Alliance itawakosa wachezaji wawili Juma Nyange na nahodha Silaji Juma kwa kupata kadi tatu za njano “Tunaamini benchi la ufundi linafanyia kazi mapungufu hayo na kujua mapema nani atachukua nafasi hiyo kwa sababu tunawachezaji wengi,” Mwafulango amesema.

Alliance walipoteza michezo miwili mfululizo ya ugenini dhidi ya Kagera Sugar kwa bao 1-0 kabla ya kupokea kichapo kizito cha mabao 4-0 kutoka kwa Mwadui FC , matokeo ambayo yanazidi kuwaweka katika nafasi mbaya, wakiwa katika nafasi ya 17 na alama zao 13 baada ya michezo 16.

Sambaza....