Sambaza....

Misimu miwili imeshakamilika akiwa katika ardhi yenye udongo mwekundu, udongo ambao upo kwenye mbuga ya msimbazi, mbuga pekee yenye mnyama mmoja yani Simba.

Mbuga hii ina malisho ambayo yana unafuu kuzidi mbuga zingine za mikoani, ndiyo maana wengi wa wachezaji hutamani sana kuishi kariakoo wakiamini ni sehemu yenye unafuu mkubwa kuzidi mikoani.

Hapana shaka pana ukweli mkubwa kuhusiana na hiki kitu, inawezekana pia kariakoo ndiko kuna timu mbili kubwa sana hapa Tanzania na zenye mashabiki wengi sana hapa Tanzania hivo kucheza hapa huwa fahari kwa walio wengi.

Ndiyo maana asilimia kubwa ya ngozi za wachezaji wetu hutamani kuvikwa na jezi za kariakoo ( Simba au Yanga), kitu ambacho siyo kibaya.

Ubaya unakuja pale mchezaji anapoamini kukanyaga Kariakoo ndiyo safari yake ya mwisho kimpira, hawezi kuiona tena hata ligi kuu ya Afrika Kusini machoni mwake.

Macho yake hujaa tongotongo nzito, masikio yake huwa na ukuta na akili yake mwisho wa siku huwa ina upofu na ukiziwi kwa wakati mmoja.

Ni ngumu kwake yeye kuona na kusikia wakati akiwa uwanjani chenga yake moja humfanya awe Mfalme wa muda na akienda mtaani ofa za bia huwa nyepesi kwake kuzipata.

Hakuna anayependa ugumu kwenye maisha haya magumu, wengi wanapenda vitu vyepesi ndiyo maana hurudi nyuma kwa sababu ya kupenda vitu vyepesi kwenye maisha yao.

Hapo ndipo umuhimu wa kuwauma sikio ndipo unapoanzia. Najua Shiza Ramadhani Kichuya mkataba wake na Simba unamalizika msimu huu.

Hapa ndipo umakini unapotakiwa utembee katika fikra zake, kuna maswali kadhaa ambayo anatakiwa kujiuliza kabla hajafanya kitu chochote.

Kwanza, malengo yake ni yapi? Kipi anakilenga kutokana na ndoto yake ? Ndoto yake ya siku zote ilikuwa ni kucheza mpira hapa nchini au katika ligi kubwa duniani?

Kama ndoto yake ilikuwa kucheza hapa Tanzania siyo dhambi kwake yeye kuamua kubaki hapa kwa sababu ndoto yake inamwelekeza hivo na lazima awe na malengo ya kutimiza ndoto yake.

Kama ndoto yake ni kucheza kwenye moja ya ligi kubwa duniani anatakiwa autazame muda kiufasaha kisha ajiulize maswali kadhaa ana miaka mingapi? na muda wa mchezaji kucheza katika kiwango cha juu ni miaka mingapi?

Shiza Ramadhani Kuchuya ana miaka 25 mpaka sasa ni umri ambao mchezaji hupevuka kikamilifu kwenye mpira, anakuwa ameshatoka kwenye umri wa ukijana na anaingia kwenye umri wa ukomavu katika mpira.

Hivo kama ana miaka 25 akiongeza mkataba na timu ya hapa Tanzania itamlazimu akae tena mwaka mmoja hapa nchini hivo itamlazimu yeye kuondoka hapa nchini akiwa na miaka 26 kuelekea 27, na hawezi kwenda moja kwa moja kwenye ligi kubwa duniani ambazo anaziota. Ataenda kwenye ligi ambayo itamsaidia kufika huko, anaweza kufika huko akiwa na umri wa miaka 29 , umri huu ni wa mwisho kwa mchezaji kucheza katika kiwango cha juu.

Hivo kipi Kichuya anatakiwa kukifanya ? Kwangu mimi naona ni wakati sahihi kwake yeye kuondoka nchini na kwenda kutafuta malisho mazuri ambayo yatamjenga kiafya ili aweze kwenda sehemu ambayo huwa anaiota kila siku.

Siyo muda sahihi kwa Shiza Ramadhani Kichuya kuendelea kubaki hapa nchini, anatakiwa akimbizwe kwa nguvu, hatutaki kumuona tena akiwa msimbazi. Magoli yake yameshatuchosha kuyaona akiyafungia hapa, hatutaki tena pasi zake za mwisho kuziona kwenye ƙligi yetu, tunachotaka kuona ni yeye akipitia njia ambayo Mbwana Samatta, Simon Msuva na Abdi Banda walipitia.

Anatakiwa aelewe ni muhimu kuwa na welekeo mzuri kuliko kasi ya kukimbia, anatakiwa kutazama mbele muda huu na siyo kuendelea kutazama sehemu ambayo alipo sasa hivi.

Sehemu aliyopo kaitumia kama sehemu ya kujiuzia, kashajiuza vya kutosha. Ana mengi bora aliyoyafanya, mengi ambayo kama akiyatumia vizuri yataweza kuwa msaada kwake yeye kutoka alipo na kusogea hatua nyingine mbele ya ziada.

Ni muda wa kukaa akiwa ametulia na washauri wake wa karibu na mawakala ambao wataangalia namna ya kutumia kipaji cha Kichuya kukipeleka mbele maana alipo sasa hivi hapamfai tena anatakiwa kuangalia kesho iliyobora kuliko Jana inayofanana na siku zote.

Sambaza....