Sambaza....

Soka ndo mchezo pendwa zaidi duniani, ni mchezo wa kushangaza wenye matokeo ya kuduwaza. Furaha na karaha majonzi na faraja vyote utavipata katika soka.

Nyakati bora za ushindi katika soka huwapa furaha mashabiki na wafuatiliaji wake na kujiona wathamani zaidi na wenye bahati, upo wakati soka litakushangaza kwa kukupa kile usichotarajia kushindwa na kupoteza huleta uchungu sana kwa wapenzi wa mchezo huu.

Wengine hujiua kukwepa fedhea wengine hukata tamaa na kukubali kushindwa wengine hudiriki kuukataa mchezo huu mzuri wengine hupata sonona isiyokoma na majonzi yasiyoisha hapo ndipo panahitajika sauti ya mfariji, mtu ambaye atang’ang’ana kuwainua na kuwakumbusha kuhusu raha na karaha za mchezo hapa ndipo mbeba bendera wa mchezo huu pendwa anahitajika ajitokeze katikati ya watu wenye huzuni na waliokata tamaa kuwakumbusha kuhusu vita ya soka (kushinda, kufungwa na sare).

Wachezaji wa Simba katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa waliindoshwa na Wydad Casablanca.

Januari tatu saa sita dakika arobaini na moja 2022 simba ilimtambulisha Ahmed Ally kuwa Afisa habari mpya wa klabu, akichukua nafasi ya Haji manara aliyeisemea Simba kwa miaka sita.

Ulikuwa wakati mgumu kwa mashabiki wa Simba kwani walimpoteza kipenzi chao ambaye aliwasemea na kuwatetea wakati wote lakini ulikua wakati mzuri na bora kwa Ahmed ally kwani Wanasimba walikuwa na bashasha na hamasa ya kutaka kujua ni nini amekuja nacho Ahmed Ally.

Kwa mda mfupi alifanikiwa kuituliza mashua iliyokuwa inayumbishwa na upepo wa Haji Manara uliokuwa unavuma kutokea jangwani.
Msimu huu Simba imepoteza  vikombe vyote na imeshindwa kufikia malengo iliyojiwekea ya kufika nusu fainali Klabu Bingwa Afrika, kubeba ndoo ya Azam Confederation na NBC Premier League.

Ahmed Ally msemaji wa klabu ya Simba Sc

Mashabiki wameikatia tamaa timu yao, viongozi ni kama hawapo mashabiki hawaelewi tena na hii inachagizwa na mafanikio ya majirani zao Yanga lakini katika wakati huu mgumu, wakati ambao Simba imevishindwa vita wafuasi wake na mashabiki wake wako hali dhoofu, buriani lunyasi, Anajitokeza Ahmed ally na bendera ya matumaini wapinzani wameshinda vita, majeshi ya wapinzani yametangaza ushindi yeye anasimama na kuinyanyua bendera ya Simba juu akiamini wakati bora unakuja hivyo wasimame tena na kupigana kwani ushindi uko karibu.

Sio kama hateseki au haumii lahasha ana moyo wa nyama na kuumia anateseka vijembe na maneno ya wapinzani hayamfanyi kuwa mnyonge. Idara ya habari anayoisimamia imesimama kidete kuwaunganisha mashabiki inawasihi na kuwasisitiza, inawataka waendelee kuiunga mkono timu yao huku wakisuka na kuweka mipango vema kwa ajili ya mapambano ya msimu ujao.

Kitengo cha habari anachokisamia hakijakaa kinyonge na hakiko nyuma, hamasa, shime na, taarifa zinahohusu klabu zinatoka kwa wakati lakini pia wanaposti video za nyakati zao bora za nyuma mfano magoli makali, ikiwakumbisha mashabiki kuwa walikua na wakati mzuri hapo nyuma licha ya sasa mambo kwenda vibaya ila wategemee mazuri.

Bendera ya ufariji, bendera ya maono, bendera ya mipango, bendera ya ushindi imebebwa na Ahmed Ally.

Sambaza....