Labda amesahau wajibu wake, ama pengine haitaji kusonga mbele zaidi ya alipo sasa, namba kumi huyu mwenye kipaji kikubwa cha kumiliki mpira, kuchezesha mshambulizi wa kwanza, kupiga pasi ‘rula’ za mwisho na kufunga magoli ya ‘video’ anapaswa kukumbushwa sasa kuwa ‘kazi yake ni kucheza soka’ na itampaisha zaidi ya vile Yanga SC ilivyotaraji kupaishwa naye.
Ibrahim AJIB kama mchezaji soka mwenye ndoto kubwa anapaswa kuachana na tabia yake ya ‘uvivu’ katika viwanja vya mazoezi, apunguze sababu zinazomfanya mara nyingi awe nje ya timu, na anazingatie ukuaji na upevukaji wake kimchezo kila baada ya dakika 90’ za mchezo unaomalizika.
Kwa mchezaji ambaye hajashinda taji lolote la ligi kuu kwa misimu sita mfululizo aliyochezea Simba SC na Yanga anapaswa kuelewa kuwa yeye si sehemu ya historia nzuri ya kukumbukwa klabuni.Ajib anapaswa kupambana sasa ili awe mshindi, na aingie katika listi ya vikosi vya mataji ya juu katika nchi.
Kwa Ajib anaweza kukumbukwa kama usajili ghali mbovu zaidi kuwahi kufanywa na Yanga kutoka kwa mahasimu wao Simba, lakini namuona bado akiwa na nafasi ya kuthibisha thamani yake ya usajili inayokadiriwa kufikia Tsh. 60 milioni. Ndiyo, Yanga walimpa kiasi hicho Julai, 2017 kwa kuamini mchezaji huyo anaweza kuja kutoa matunda na msaada katika safu yao ya mashambulizi.
MABAO MATANO MSIMU MZIMA TPL…..
Goli maridadi sana la mkwaju wa mbali uliokufa ‘freekick’ katika uwanja wa Sabasaba, Njombe liliipa Yanga ushindi wao wa kwanza katika ligi msimu uliopita. Baada ya kufunga Ajib alishangilia kwa stahili ya kuvua jezi yake na kuwaonyesha watazamaji namba ya jezi yake na jina mgongoni ‘ 10 Ajib’.
Pasi murua ya mwisho ambayo ilizalisha goli la Obrey Chirwa katika mchezo ambao Yanga iliichapa Kagera Sugar FC katika uwanja wa Kaitaba ilikuwa ni jambo ambalo Ajib lilimkuza zaidi kwa mashabiki wa Yanga. Walimtazama kama ‘mwokozi mpya.’
Alifunga, Sabasaba Stadium, Njombe 0-1, akafunga na kusaidia goli la Chirwa katika Kagera Sugar 1-2, akaendeleza ufungaji mfululizo katika uwanja Kambarage, Shinyanga wakati Yanga ilipopata ushindi wao wa kwanza mkubwa msimu uliopita Stand United 0-4 Yanga, Ajib alikuwa msaada uliohitajika na kutoa matunda mazuri Yanga hasa baada ya Mrundi, Amis Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma kuumia.
Alitengeneza urafiki mzuri wa kiuchezaji na Chirwa nah ii ndiyo sababu ambayo Yanga iliweza kusawiza goli la Simba baada ya dakika tatu tu kufuatia Shiza Kichuya kuifungia Simba katika mchezo wa kwanza msimu uliopita. Lakini baada ya mchezo huo, Ajib hajawahi tena kuwa mchezaji mwenye matarajio ya kuipaisha Yanga.
MVIVU WA MAZOEZI…..
Mara baada ya kupiga pasi nyingi mbovu, kupoteza mpira-kunyang’anywa mguu na mchezo wa kurudisha pasi nyuma dhidi ya Wahabesh, Dicha FC katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam niliandika post ya kumkosa Ajib na kati ya wachangiaji waliojitokeza kuchangia alikuwa ni Juma Ndabile-mmoja wa mawakala wa soka nchini wanaotambulika na Fifa.
Ndabile alikuwa aki-muonga pia Ajib, alisema sababu kubwa iliyomfanya kuachana na Ajib ni uvivu wa mchezaji huyo. Alisema, Ajib ni mchezaji anayejiona amemaliza kila kitu katika soka na hana tamaa tena. Hataki mazoezi jambo ambalo limekuwa likimporomosha kimpira siku hadi siku na licha ya kuambiwa hajirekebishe mchezaji huyo ameonekana hayupo tayari.
Mara baada ya kiwango chake kibovu vs Dicha FC katika Caf Confederations Cup mwezi April, Ajib alipoteza nafasi yake kwa kijana Yusuph Mhilu ambaye licha ya kwamba ni kijana asiye na uzoefu wakati mwingi alikuwa bora kando ya Mzambia, Chirwa hata wakati alipotakiwa kuongoza mashambulizi kama straika pekee.
ANAWEZA KUREJEA NA KUTISHA ZAIDI YA MATARAJIO….
Uvivu wa Ajib ulImporomosha kimpira lakini si hivyo tu alipoteza nafasi katika timu ya Taifa na ameendelea kuwapoteza mashabiki wa Yanga ambao waliamini anaweza kuwabeba. Ameanza msimu huu chini ya kocha mpya, Mcongoman, Zahera Mwinyi kama mchezaji wa akiba ambaye aliingia uwanjani akitokea benchi katika mchezo pekee wa Yanga hadi sasa; Yanga 2-1 Mtibwa Sugar FC na alibadilisha sana mchezo.
Hii inaonyesha na kuleta matumaini mengine mapya kuwa mchezaji huyo anaweza kujiamsha na kubadili mwenendo wake mbaya hasa ukizingatia kocha wake amekuwa akisema mara kadhaa na kusifia kipaji chake akisema ni cha pekee- ndiyo anakipaji cha pekee lakini sasa Zahera anasifia ‘makombo’ tu ya Ajib aliyekuwa akichipukia.
Wakati akiendelea kukua kiumri, huku tayari akiwa katika maisha ya ndoa, Ajib anaweza kurejea juu kama tu ataachana na uvivu, kujiongeza kiuzoefu kila anapoongeza namba ya idadi ya michezo yake. Apunguze kupoteza mpira na upigaji wake wa pasi mbovu. Huyu ni namba kumi ambaye anaweza kuwa mpishi mzuri wa Mcongo Makambo.