MSHAMBULIZI Salum Aiyee yupo mbioni kukamilisha usajili wake wa kutoka Mwadui FC na kujiunga Yanga SC wakati huu klabu mbalimbali nchini zikiimarisha vikosi vyao.
Aiyee ni pendekezo la kocha Mwinyi Zahera na huenda mshambulizi huyo aliyefunga magoli 17 katika ligi kuu na mengine mawili katika michezo ya ‘play off’ kuwania kutoshuka daraja atakuwa ni mshambulizi wa kwanza kati ya wawili wazawa ambao kocha huyo Mcongo amependekeza.
NI BAHANUNZI MPYA……
Unamkumbuka mshambulizi Said Bahanunzi ambaye alijiunga Yanga katikati ya mwaka 2012 akitokea Mtibwa Sugar FC na kufanya mambo makubwa katika michuano ya Cecafa Kagame Cup, Julai, 2012.
Bahanunzi alikuwa ni mshambulizi mwenye uwezo mkubwa wa kucheza eneo la mashambulizi akiwa pekee ‘mshambulizi huru’, alikuwa na uwezo mzuri wa kukokota mpira, kupokea pasi na kugeuka akielekea mbele aliibuka mfunmgaji bora katika Kagame Cup 2012 licha ya kwamba alikuwa ndio kwanza amejiunga Yanga.
Sababu za nje ya uwanja – kupenda maisha ya ustaa, majeraha yalimpoteza haraka Bahanunzi na ligi ilipoanza msimu wa 2012/13 mchezaji huyo hakuwa na msaada wowote kwa klabu yake. Aliichezea hadi msimu wa 2013/14 ambao hakuongezewa mkataba mpya.
Ukitazama mbio za Aiyee, vile anavyopokea mpira, anavyotengeneza/ kujitengenezea nafasi, kujipanga katika maeneo ya hatari ya wapinzani na namna alivyo na shabaha ya kulenga lango ni wazi kijana huyu anaweza kuisaidia Yanga hasa katika eneo la ufungaji ambalo ukitoa Mcongo, Heritier Makambo Yanga ilisumbuliwa mno na tatizo la mfungaji asilia.
Kama atajibidiisha na kujiendeleza vizuri chini ya Zahera, bila shaka Aiyee atakuwa ni zaidi ya Bahanunzi na kwa kiasi kikubwa ataifungia Yanga magoli muhimu kwa sababu huyu ana nidhamu na usongo wa kutaka kufanikiwa zaidi ya Bahanunzi ambaye baada tu ya kushinda tuzo binafsi ya ufungaji bora wa Kagame Cup hakujibidiisha tena katika viwanja vya mazoezi zaidi akawa mtu wa kujirusha zaidi.