LICHA ya pambano lao la Alhamis wiki iliyopita dhidi ya Yanga SC kuingiza idadi kubwa ya mashabiki katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha wachezaji wa timu ya African Lyon walizuiliwa kwa siku nne katika hotel waliyokuwa wamefikia.
Lyon walichapwa 0-1 katika mchezo huo waliokuwa wenyeji na lengo kuu la kuhamisha mchezo huo kutoka Dar es Salaam hadi Arusha ilikuwa ni kuhakikisha timu hiyo ya Dar inavuna mapato mengi.
” Hali ya kiuchumi ni mbaya, hivi tunavyozungumza ndiyo kwanza tumefika Dar baada ya kuzuiliwa hotelini kwa siku nne kutokana na madeni ambayo klabu inadaiwa tangu tulipofika Arusha.” kinasema chanzo cha habari hii kilichoomba hifadhi ya jina lake.
” Tulitegemea kupata kitu chochote baada ya mchezo wetu na Yanga kuingiza watazamaji wa kuridhisha, lakini huwezi kuamini licha ya mashabiki kujitokeza kwa wingi lakini hakuna mapato ya kuridhisha.”
Lyon walikuwa Arusha kwa wiki nzima na licha ya mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Yanga, Jumapili iliyopita waliikabili Arusha United katika hatua ya 32 bora ya michuano ya FA ambayo wamesonga mbele kufuatia ushindi wa 2-0 katika uwanja huo wa Amri Abeid.