Klabu ya soka ya African Lyon imesema haiwezi kuzungumza lolote kuhusu kuondoka kwa Haruna Moshi Boban ambaye anahusishwa na kujiunga na Yanga SC Kwani bado hawana uhakika na usajili huo na zingine.
Meneja wa kikosi cha African Lyon Adam Kipatacho amesema watanzania wanatakiwa wasubiri tamko rasmi kutoka Jijini Dar es Salaam kama Boban ameshaondoka na kujiunga na timu nyingine.
“Mpaka leo bado hatujathibitsha mchezaji yoyote kuondoka, kwa sababu Bado hatujafuatwa kuambiwa fulani kaondoka, bado tunasubiri turudi Dar es Salaam na kuangalia ripoti ili tujue nani kaondoka na nani kabaki, mpaka sasa hivi hatujajua nani katoka,” amesema
African Lyon waliondoka Dar bila ya wachezaji wake muhimu akiwemo Haruna Moshi Boban ambaye kwa mujibu wa kiongozi wa ndani wa African Lyon ni kwamba amekuwa akichagua mechi za kucheza na hata kuanza kujifikiria kuwa yeye tayari ni mchezaji wa timu kubwa.
Kuhusu usajili wa wachezaji wapya Kipatacho amesema mpaka sasa kuna wachezaji 12 ambao wamewasajili katika dirisha dogo la usajili na imani yao ni Kuwa watawasaidia kuirudisha African Lyon katika kiwango kizuri na hawatashuka daraja.
“Kushuka daraja ni ngumu sana, kwa sababu tunawachezaji takribani 12 tumesajili hapa hivi tunasubiri usahili ufanyike na tarehe 15 wapitishwe utaona timu inabadilika zaidi ya hapa,”
Kipatacho ameyazungumza hayo mara baada ya mchezo wa ligi dhidi ya Mbao FC uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba na kumalizika kwa sare ya 0-0.