Baada ya jana mtandao huu kukuletea taarifa ya Yanga kumtaka Abdulhalim Humoud kutoka katika klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro na viongozi kukaribisha mazungumzo kati yao na klabu inayomtaka.
Kupitia Afisa Habari wa klabu hiyo Thobias Kifaru , amezidi kuuambia mtandao huu kuwa klabu hiyo ya Mtibwa Sugar iko katika harakati za wao kuwaongezea mikataba wachezaji ambao mikataba yao inaelekea mwisho.
“Kwa sasa tuko kwenye mazungumzo ya kuwaongezea mikataba wachezaji ambao mikataba yao inaelekea kuisha na mazungumzo yanaenda vizuri , ingawa kuna wachezaji wengine ambao wana mikataba mirefu mpaka mwaka 2022”- alisema Afisa habari huyo mkongwe.
Kuhusu Abdulhalim Humoud, Afisa habari huyo alidai kuwa kwa sasa timu inayomwihitaji waje kuzungumza na Mtibwa Sugar ingawa awali vilabu hivi vilimterekeza Abdulhalim Humoud.
“Walimterekeza awali , aliwahi kupita Simba na Azam FC lakini wakamterekeza sisi tumemchukua na kumfanya arudi kwenye kiwango kikubwa kwa sasa pamoja na kwamba awali aliterekezwa na vilabu hivi” – alisema Afisa Habari huyo wa Mtibwa Sugar .
Aidha, Afisa Habari huyo amedai kuwa wao kama Mtibwa Sugar wangependelea zaidi Abdulhalim Humoud angeenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ili kuitangaza zaidi Mtibwa Sugar.
“Baada ya wao kumterekeza na sisi tukaamua kumrejesha katika kiwango chake kikubwa tungetamani zaidi Abdulhalim Humoud kwenda soka la kulipwa nje ya nchi ili aitangaze Mtibwa Sugar kuliko kwenda sehemu ambayo walimterekeza awali”- alimalizia Afisa habari huyo wa Mtibwa Sugar