Nahodha wa timu ya soka ya Mbao ya jijini Mwanza, Robert Ndaki amewaomba mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu na kutotegemea makubwa kutoka kwao kipindi hiki ambacho wanafanya vizuri bali wanachotakiwa ni kuwaombea na kuwaunga mkono kwa kila mchezo wa ligi.
Ndaki amesema matokeo ambayo wanazidi kuyapata si kwamba ndio wataendelea kufanya vizuri hadi mwisho wa ligi bali umoja na mshikamano wa pamoja ndio utakaowasaidia kufanya vizuri msimu huu tofauti na misimu mingine.
“Mashabiki wanatakiwa kuwa wavumilivu, ligi ni ngumu sisi tutaendelea kupambana, ili kuupambania mkoa wetu, hata ubingwa tunaweza kuchukua kwa maana hakuna aliyesema hii ligi ni kwa ajili ya Simba ama Yanga hapana, timu yoyote ambayo imejiandaa inaweza kuwa bingwa,”
Amesema wao watajitahidi kufanya vizuri katika kila mchezo kwani hawachezi michezo yote 38 kwa pamoja bali kila mchezo una siku yake na hilo ndilo ambalo watafanya kuhakikisha kila mchezo wanapata matokeo.
“Kwa sisi hatuna michezo mingi, tuna approach mchezo mmoja mmoja kwa sasa tunaangalia Coastal Union na baada ya hapo tutaangalia mchezo unaofuata kwa maana hakuna siku ambayo tutacheza michezo mitatu, na sisi hatushindani na timu ambazo zipo mbele yetu, sisi tunacheza ligi yetu maana kila mechi sisi tunaona tukifanya vizuri tunajitengenezea mazingira mazuri,” amesema.
“Kila timu iwe tayari kutupokea kwa maana sisi tunakuja kitofauti, nadhani hata mashabiki wanatuona tumekuja kitofauti, lakini pia wasitarajie makubwa sana kutoka kwetu,” Ameongeza.
Ndaki ambaye alifunga katika dakika za lala salama kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons na kuwapa Mbao ushindi wa pili mfululizo kwenye uwanja wa CCM Kirumba, amesema kwa sasa malengo yao ni kuhakikisha wanaibuka na ushindi dhidi ya Coastal Union katika mchezo mwingine wa ligi.
Mpaka sasa Mbao FC wameshacheza michezo sita na kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika ligi yenye timu 20 kwa kukusanya alama 13, alama moja mbele ya Mabingwa wa kihistoria Yanga, na alama tatu zaidi ya Mabingwa watetezi Simba Sports Club.